Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Josephat Maganga akiongea na wanamichezo katika uwanja wa shule ya sekondari Dodoma
Idadi ya vikombe vilivyochukuliwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika UMISSETA ngazi ya Mkoa
Wanamichezo wa UMISSETA Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
*******************************
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
TIMU ya Mkoa wa Dodoma itakayoshiriki mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Sekondari (UMISSETA) kitaifa imetakiwa kushiriki mashiondano hayo kwa nidhamu ili kuibuka na makombe mengi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Josephat Maganga alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakati kufunga mashindano ya UMISSETA ngazi ya mkoa wa Dodoma yaliyofanyioka katika viwanja vya shule ya sekondari ya Dodoma leo mchana.
Maganga aliwapongeza walimu wa michezo kwa kuchagua timu nzuri ya Mkoa wa Dodoma itakayoshiriki UMISSETA taifa mkoani Mtwara. Aidha, aliwapongeza wanafunzi waliochaguliwa kuunda timu ya Mkoa wa Dodoma na kusema kuwa wamefanya kazi kubwa kufikia hatua hiyo. ”Niseme jambo moja, nalo ni kuwapongeza kwa jitihada mliyoonesha na nidhamu katika mashiondano haya jambo lililowarahisishia walimu kuchagua timu nzuri. Wanafunzi ambao hamkuchaguliwa katika timu ya mkoa, msisononeke. Wote mmefanya vizuri ila ilikuwa lazima kufanya mchujo sababu nafasi ni chache” alisema Maganga.
Mkuu huyo wa Wilaya ya Dodoma mjini aliwakumbusha wanamichezo hao kuwa wamebeba dhamana kubwa ya Mkoa wa Dodoma. “Nendeni mkacheze kwa weledi. Mkacheze kwa nidhamu ya hali ya juu na kutetea ushindi. Tunasubiri zawadi ya makombe katika mashindano hayo” alisisitiza Maganga.
Kwa upande wake, kepteni wa timu ya mpira wa kikapu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliyoibuka na kombe la mchezo huo, Gervas Fred alisema kuwa siri ya mafanikio ni ushirikiano na kucheza kwa umoja kama timu. Alisema kuwa mafunzo mazuri ya kocha wao yalikuwa chachu ya mafanikio katika michezo yote waliyoshiriki.