Dkt Ali Mzige akionesha bango lenye picha ya mtu aliathirika kutokana na kuvuta sigara
Dkt Ali Mzige akiwaonesha waandishi wa habari bango lililoandikwa madhara mbalimbali ya matuminzi mabaya ya chakula
Dkt Ali Mzige akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wake khusu ulaji mbaya wa chakula.
Na Mwandishi Wetu, Korogwe
ULAJI mbaya wa chakula, usiozingatia kanuni za kiafya, unaweza kuchangia magonjwa mbalimbali katika mwili wa binadamu na hivyo imeshauriwa watu wabadili taratibu za mlo kila siku.
Akizungumza katika Kongamano la afya lililokuwa na kauli mbiu ‘Pima afya yako kabla hujaugua,’ Mkurugenzi wa Zahanati ya Manundu, Dkt Ali Mzige alisema ulaji mbaya wa chakula unaweza kusababisha magonjwa ikiwemo saratani.
Dkt Mzige ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Kinga na Tiba wa Wizara ya Afya, alisema magonjwa mengi kama kisukari, shinikizo la damu na saratani husababishwa na watu kutozingatia kanuni za chakula wanachokula.
Akashauri watu wapunguze nishati lishe za ziada (extra calories) matumizi ya sukari, mafuta yenye lehemu (cholesterol) na chumvi.
“Tutumie vyakula vya asilia vyenye lishe makapi-fibre, kula dona badala ya sembe nyeupe, mihogo, magimbi, viazi vitamu vikipikwa kwa kuchemshwa bila kukaangwa ni bora kuliko chips,” alisema Dkt Mzige.
Akatolea mfano walaji wa nyama ya nguruwe maarufu ‘Kiti Moto’, wanauwezekano wa kupata tatizo la kifafa linalotokana na tegu inayokimbilia kwenye ubongo.
Alisema nyama hiyo pia inasababisha magonjwa takribani 17 ambayo kwa watumiaji wa ARVs dawa hizo zitashindwa kufanya kazi sawasawa kutokana na uwepo mkubwa wa asidi.
“Nyama ya nguruwe siyo white meat, hilo wajue lakini nyama hii ina magonjwa karibu 17 na husababisha madhara makubwa kwenye mwili,” alisema Dkt Mzige na kuongeza kwamba ulaji wa mbogamboga unasaidia kuondoa sumu mwilini.
Aidha, alitoa tahadhari kwa akina mama wajawazito wanaopendelea kula chips mayai wakati wa mimba kwamba chakula hicho kitawapa uwezekano wa kupata kisukari cha mimba.
Pia alishauri akina mama wanaotengeneza unga wa lishe kwa ajili ya watoto kwamba unga huo uliokuwa na aina nyingi za nafaka haufai kwa matumizi ya watoto.
Dkt Mzige alitambulisha kituo chake kipya cha Mshangai Preventive Medical Care Polyclinic, itakayokuwa na jopo la madaktari bingwa watatoa huduma zote za magonjwa yanayotokana na matatizo mbalimbali ikiwemo saratani.