************************
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imekutana na wadau wa sekta ya kilimo mkoani Morogoro kujadili namna ya kuboresha uzalishaji wa nguvukazi yenye ujuzi wa stadi za kilimo kupitia programu ya Uanagenzi Pacha (Dual Apprenticeship Training System, DATS).
Akizungumza wakati wa warsha iliyofanyika katika chuo cha VETA Kihonda mkoani Morogoro, tarehe 13 Aprili, 2021, Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Mashariki, Asanterabi Kanza alisema tafiti za soko la ajira katika mkoa wa Morogoro zimeonyesha mahitaji makubwa ya watu wenye stadi za kilimo hasa kwenye eneo la uendeshaji wa mitambo ya kilimo na ufundi wa zana za kilimo.
Alisema VETA imekuwa ikitoa mafunzo ya ufundi wa zana za kilimo kwenye vyuo vyake na kwa sasa wameona umuhimu mkubwa wa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo katika kutoa mafunzo kupitia programu ya Uanagenzi Pacha ambayo inampa fursa kijana kupata ujuzi wa fani husika akiwa chuoni na sehemu ya kazi, hivyo kumwezesha kwa kiasi kikubwa kujifunza kwa vitendo na kuendana na mahitaji ya soko la ajira pamoja na kupata uzoefu na uelewa wa mazingira halisi ya kufanyia kazi.
“VETA inatambua umuhimu wa kushirikiana na waajiri kwenye sekta mbalimbali kutoa mafunzo kwa kuwa ushirikiano huo unawezesha kuandaa nguvu kazi mahiri zaidi inayoendana na mahitaji halisi ya viwanda hasa kwa kuzingatia kuwa sehemu kubwa ya mafunzo hayo yanafanyika sehemu za kazi.”Alisema
Aliwaasa wadau wa kilimo mkoani Morogoro kushirikiana kwa karibu na VETA kutoa mafunzo hayo ili kuweza kupata vijana bora zaidi na wenye weledi wa kutosha katika kuongeza tija kwenye kilimo.
Naye Mratibu wa Programu hiyo, Francis Komba alisema pamoja na mambo mengine, warsha hiyo imelenga kuwajengea uwezo wasimamizi wa mafunzo hayo viwandani, juu ya namna bora ya kutekeleza programu hiyo na kubadilishana uzoefu.
“Waajiri wamefurahia mfumo huu na wameonyesha mwitikio mkubwa kwa kuwa imewapa tumaini la kupata wafanyakazi wenye ujuzi kwani kwa sasa watu wenye ujuzi ni wachache hasa katika sekta ya Ufundi wa zana za kilimo.” Alisema
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Kibaigwa Flour Supplier Ltd, Sebastian Msolwa, amepongeza mfumo huo na kusema utakuwa mkombozi kwao kwani wamekuwa wakipata changamoto ya watu wenye ujuzi wa kufanya matengenezo kwenye mitambo yao pindi inapopata hitilafu.
Kwa upande wake Meneja Mafunzo wa Kampuni ya Kilombero Sugar, Abdulhamid Masai alishauri VETA kuongeza kozi nyingi zaidi kwenye mfumo wa Uanagenzi Pacha ili kukidhi mahitaji ya nguvukazi yenye ujuzi kweye sekta nyingi zaidi.
Mfumo wa utoaji mafunzo wa Uanagenzi Pacha unahusisha kuhudhuria mafunzo ya vitendo kwenye karakana na darasani kwenye vyuo vya VETA kwa upande mmoja na mafunzo ya vitendo zaidi katika sehemu za kazi kwa upande mwingine. Mafunzo hayo ni ya miaka mitatu ambapo kwa kila mwaka mwanagenzi anatumia wiki 20 VETA na wiki 32 kwa mafunzo ya viwandani.
Mfumo wa mafunzo ya Uanagenzi Pacha ulianzishwa mwaka 2011/12 kwa ushirikiano kati ya VETA na Hamburg Chamber of Crafts (HWK) ya Ujerumani, ambapo kwa sasa unatekelezwa katika vyuo vinne vya VETA vya Moshi RVTSC (Ukarimu na Utalii), Dar es Salaam RVTSC (Ufundi Umeme na Ufundi Magari), Simanjiro DVTC (Uashi) na Manyara RVTSC (Ufundi wa Zana za Kilimo). Viwanda na kampuni zaidi ya 150 zimenufaika na mafunzo hayo.