Home Mchanganyiko MASHIRIKA YASIYOKUWA YA KISERIKALI NA WADAU WA ASAS ZA KIRAIA WAKUTANA KUJADILI...

MASHIRIKA YASIYOKUWA YA KISERIKALI NA WADAU WA ASAS ZA KIRAIA WAKUTANA KUJADILI SHERIA NA MIONGOZO INAYOZISIMAMIA

0

Kiwanga Mkurugenzi mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS).

………………………………..

Foundation for Civil Society (FCS) kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Serikali (TANGO) pamoja na Shirika la Equality for Growth (EfG) yamekutanisha wadau mbalimbali kutoka asasi za kiraia kwa lengo la kujadili matakwa ya sheria na miongozo inayosimamia na kuratibu sekta ya Asasi za Kiraia nchini Tanzania baada ya sheria hizo kufanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Mkutano uliofanyika kwa siku mbili, tarehe 30-31 Machi mwaka hu una ulifanyika kwa njia ya mtandao na kuwakutanisha wadau mbalimbali zikiwemo Asasi za Kiraia (AZAKI) mbalimbali nchini na AZAKI zinazowezeshwa na FCS kwa lengo la kutoa elimu juu ya utekelezaji wa Sheria hizo , kuzipitia ili kuona namna ambavyo zitatekelezwa sambamba na kutoa fursa kwa wadau hao kutoa maoni yao.

Akizungumza hivi karibuni katika Mkutano huo, Meneja Idara ya Kujenga Uwezo FCS ,Edna Chilimo amesema kuwa mkutano huo uliwakutanisha jumla ya Asasi za kiraia 300 ambapo mada mbalimbali zilitolewa na baadhi ya wataalamu kutoka katika Ofisi ya usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) Usajili wa Jumuiya za Kijamii, na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ikiwa na lengo la kutoa elimu na uelewa mpana kwa Asasi hizo kuhusu maboresho ya Sheria hizo.

“Kuna chanagamoto kubwa katika uelewa na tafsiri ya sheria hizo, wapo wengine walikuwa hawazielewi na wengine walikuwa na tafsiri potofu, wengine walihamaki hivyo FCS kama Mwezeshaji baada ya kugundua tatizo tukashirikiana na wadau wengine ambao ni Mashirika ya kimtandao ambayo ni NaCoNGO, TANGO na EQUALITY FOR GROWTH (EfG) kutengeneza Programu ya kuwawezesha Asasi za kiraia kuelewa sheria hizo vizuri na wapate tafsiri sahihi ili mwisho wa siku waweze kuzifuata na kuzifanyia kazi ili waweze kutekeleza miradi yao kwa weledi wakiwafikia wananchi na kuhakikisha wanafuata sheria hizo ” amesema Edna.

Aidha amefafanua kuwa katika programu hiyo licha ya kutoa elimu ya kuwajengea uwezo wa uelewa wa Sheria hizo pia inalenga kutoa msaada kwa yale mashirika yaliyokuwa yanahitaji msaada wa kitaalamu ili waweze kuelewa zaidi ili kila mmoja aweze kufikia malengo.

“Programu hii tunaifanya kwa karibu na watu wa Serikali kwakuwa wao ndio wasimamizi wa hizo sheria hivyo tumefanya kazi na Ofisi ya msajili wa NGOs, Ofisi ya Msajili wa Jumuiya na Ofisi ya Msajili kutoka RITA ambao walipata nafasi nzuri sana ya kufafanua mambo mbalimbali yanayohusu AZAKI kuanzia kusajiliwa, namna ya kufuata Sheria na Sheria zenyewe, kwa hiyo itawasaidia sana wadau kuweza kufahamu maeneo tofauti ya kufanya kazi kwa kufuata Sheria” amefafanua.

Ameongeza kuwa FCS inajipanga kuandaa mkutano mkubwa zaidi kwa kushirikisha wadau wengi ili kuendelea kutoa uelewa juu ya sheria hizo kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali kutoka katika Taasisi za Serikali kama TRA, NSSF, OSHA, WIZARA YA KAZI na Taasisi nyingine za Serikali ili kuendelea kukuza uelewa mpana zaidi.

Kwa upande wao baadhi ya Asasi za Kiraia zilizoshiriki mkutano huo zimesema kuwa zimepokea maboresho ya Sheria hizo na kwamba wanahakikisha wanafuata sheria inavyosema.