Diwani Kata ya Mbagala Kuu, Shabani Othman Abubakari enzi za uhai wake.
Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, Shabani Othman Abubakari, akizungumza na walimu wote wa shule za msingi na sekondari za kata hiyo enzi za uhai wake.
Na Dotto Mwaibale
DIWANI wa Kata ya Mbagala Kuu Shabani Othman Abubakari (CCM) amefariki dunia katika moja ya nyumba ya kulala wageni iliyoyopo Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam alipokuwa na mwanamke anayedaiwa ni mchepuko wake.
Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Abdallah Mtimika na kuwa mazishi yake yatafanyika leo katika makaburi ya Tanita yaliyopo eneo la Kibonde Maji.
Mmoja wa wahudumu nyumba hiyo ya kulala wageni (jina lake linahifadhiwa) alisema diwani huyo alifika akiwa na gari lake wakiwa na msichana huyo usiku wa kuamkia juzi na kuchukua moja ya chumba katika nyumba hiyo.
Alisema asubuhi baada ya kuamka wakati akifanya usafi ndipo alipoukuta ufunguo wa chumba alichokuwa amekichukua diwani huyo na msichana huyo ukiwa umetupwa chini ambapo alishituka na kwenda katika chumba hicho na kukuta kikiwa kimefungwa na kilipofunguliwa walimkuta diwani huyo akiwa amefariki lakini yule msichana waliyekuwa naye hayupo.
Muhudumu huyo alisema baada ya kuona tukio hilo walitoa taarifa polisi ambao walifika na baada ya kuwahoji waliuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke ili kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba baada ya kupigiwa simu yake mara kadhaa ikawa inaita bila ya kupokelewa.