Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas akitoa uthibitisho kwa waandishi wa habari kuwa Marais wa nchi zaidi ya 10 wanatarajiwa kuwa sehemu ya viongozi watakaohudhuria tukio la kutoa heshima za mwisho kwa Hayati Dk.John Magufuli litakalofanyika kesho Machi 22,2021 uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Muonekano wa sehemu ya viongozi watakapo tutoa heshima za mwisho kwa Hayati Dk.John Magufuli litakalofanyika kesho Machi 22,2021 uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Baadhi ya watu waliohudhuria kuangalia maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kwa Hayati Dk.John Magufuli kesho Machi 22,2021 uwanja wa Jamhuri Dodoma.
…………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
TUNAKUJA Kumsindikiza Shujaa wa Afrika! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Marais wa nchi zaidi ya 10 wanatarajiwa kuwa sehemu ya viongozi mbalimbali kutoka nje ya Tanzania watakaohudhuria tukio la kutoa heshima za mwisho kwa Hayati Dkt. John Magufuli litakalofanyika kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Uthibitisho huo umetolewa leo Machi 21,2021 jijini Dodoma na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa maraisi hao ni kutoka nchi za Kenya, Malawi, Commoro, Msumbiji, Zimbabwe, Zambia, Namibia, Botswana, Afrika Kusini na DR Congo.
Dk Abbas amesema pamoja na marais na wakuu hao wa Nchi 10 ambao wamethibitisha kuwepo Dodoma hiyo kesho pia wawakilishi kutoka Asasi za Kikanda na Mabalozi zaidi ya 50 wamethibitisha kuwepo katika shughuli hiyo ya maziko ya kitaifa.
Rais wa Rwanda amemtuma Mwakilishi wake ambaye ni Waziri Mkuu wake, Rais wa Angola amemtuma Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi hiyo kumuwakilisha wakati Rais wa Burundi amemtuma Makamu wake wa Rais kumuwakilisha.
” Mwili wa mpendwa wetu Hayati Dk Magufuli utawasili jioni ya leo hapa Dodoma na utaelekea Ikulu Chamwino ambapo wananchi wa jiji la Dodoma mnaombwa kujitokeza barabarani wakati mwili ukipita ili tumpe heshima kiongozi wetu.
”Mara baada ya kuwasili mwili huo utaelekea Ikulu ya Chamwino kwa kupitia barabara za Chako ni chako, Barabara ya Nyerere, Round about ya Mkuu wa Mkoa, Bunge, Morena, Bwigiri- Chamwino-Ikulu, wanachi wote wa maeneo haya wanaombwa kujipanga kwenye barabara hizo kutoa heshima zao”amesema Dk. Abbas
Dk.Abbas amesema kuwa siku ya kesho Mwili utatoka Ikulu Chamwino utaanzia bungeni ili wabunge wapate fursa ya kumuaga kiongozi wetu na baadaye mwili utakuja hapa uwanjani, baada ya viongozi kuaga wataanza kuaga wananchi na tutajitahidi wage hadi usiku kwasababu ni siku moja tu.
Siku ya Kesho kama ambavyo ilitangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan itakua ni mapumziko na tunakumbusha tena siku ya Machi 26 ambayo ndio tutampuzisha kiongozi wetu pia itakua siku ya mapumziko kitaifa, ” Amesema Dk Abbas.