Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Dunstan Kitandula leo Machi 12, 2021 imefanya ziara kukagua utekelezaji wa Mradi wa kimkakati wa Julius Nyerere (JNHPP) Mw 2115.
Akiongea katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Dunstan Kitandula amesema Kamati imekagua maeneo manne ya utekelezaji wa Julius Nyerere na imeridhishwa na hatua ambayo mradi umefikia.
“Jinsi ujenzi unavyoendelea inakwenda kama tulivyoongea, haya ni mafanikio makubwa sana, nafurahi hata malipo kwa Mkandarasi yamelipwa kwa wakati na hatudaiwi kwa kazi aliyofanya kulingana na mpango kazi” amesema Mhe. Kitandula.
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha mradi wa Julius Nyerere unatekelezwa.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema tangu kuanza kutekelezwa kwa mradi wa Julius Nyerere Mkandarasi amekuwa akilipwa kulingana na mpango kazi.
Aliongeza hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa takribani Trilioni 2.04 ambayo ni sawa ya asilimia 100 ya kazi aliyoifanya.
“Sisi kama Serikali tumejipanga kuusimamia Mradi wa Julius Nyerere usiku na mchana na utakamilika mwezi Juni 2022, kwasasa umefikia asilimia 43 ya utekelezaji wake” amesema Dkt. Kalemani.
Aliongeza kukamilika kwa mradi wa Julius Nyerere mwezi Juni 2022 pamoja na miradi mingine inayotekelezwa Nchi itakuwa na jumla ya megawati 4,478 ambazo zitakuwa chachu ya maendeleo.