Home Mchanganyiko ASKARI WAHAMISHWE URAIANI-KAMATI YA BUNGE

ASKARI WAHAMISHWE URAIANI-KAMATI YA BUNGE

0

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama  kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida.Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambae pia ni Mbunge wa Ilala,Mussa Azan Zungu.Ziara hiyo imefanyika leo mkoani Singida.

Mtaalamu wa Ujenzi wa Jeshi la Polisi akitoa maelekezo ya Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya Jeshi la Polisi mkoani Singida leo.Wapili kushoto  ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambae pia ni Mbunge wa Ilala,Mussa Azan Zungu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama waliofika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kabla ya kuanza ziara ya kukagua miradi ya Jeshi la Polisi iliyoko mkoani Singida.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Khamis Hamza Chilo akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama waliofika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida kabla ya kuanza ziara ya kukagua miradi ya Jeshi la Polisi iliyoko mkoani Singida.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

………………………………………………………………………………

Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama imeishauri  Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi nchini  kutumia Mfumo wa Fedha za Tuzo na Tozo katika kuendesha miradi mbalimbali ya jeshi hilo ambayo uzoefu unaonyesha miradi  mingi iliyotumia fedha hiyo kukamilka huku kamati hiyo ikisisitiza ujenzi wa nyumba za askari ili kuwaondoa askari polisi uraiani.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo,ambaye pia ni Mbunge wa Ilala,Mussa Azan Zungu baada ya ukaguzi wa miradi miwili ya Jeshi la Polisi ikiwemo Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida na Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Kikosi cha FFU Pamoja na ghala la silaha.

“Mtumie Mfuko wa Tuzo na Tozo kujenga nyumba za maafisa na askari,mpunguze maaskari kukaa uraiani,wakikaa uraiani kuna matatizo makubwa wanazoeana sana na wananchi na askari eneo lake ni kambini sio kukaa nje ya kambi” alisema Zungu

Mbunge Zungu pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,George Simbachawene na Inspekta Jenerali wa Polisi,Simon Sirro kwa kusimamia Pamoja na kukamilisha miradi mbalimbali ndani ya jeshi hilo.

Akizungumza katika ziara hiyo,Mshauri wa Ujenzi wa Jeshi la Polisi nchini,Naibu Kamishna Richard Malika alitaja gharama ya Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Kamanda ambapo mpaka mradi kukamilika utagharimu Shilingi Bilioni 1.2 huku akiweka wazi gharama hizo kutoka katika mfuko wa tuzo na tozo uliopo chini ya Inspekta Jenerali wa Polisi,Simon Sirro.