Na Catherine Sungura WAMJW – Mbeya
Serikali imelenga kuziwezesha Hospitali zote za Rufaa za Mikoa (26) nchini ili kuweza kuanzisha huduma za matibabu ya ugonjwa sugu wa figo ikiwemo usafishaji damu ifikapo mwaka 2025.
Yamebainishwa hayo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima alipotembelea Kitengo cha usafishaji damu kwa wagonjwa wa figo (hemodialysis) katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Nyanda za Juu Kusini (MZRH), kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani yanayofanyika hapo kesho ulimwenguni kote.
“Wizara tumeongeza huduma za Kibingwa katika Hospitali zetu ambapo kwa sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali zote za Rufaa za Kanda na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tanga – Bombo, zinatoa huduma ya usafishaji damu.
“Serikali imelenga kuziwezesha Hospitali zote za Rufaa za Mikoa (26) nchini ili kuziwezesha kutoa huduma za matibabu ya ugonjwa sugu wa figo ikiwemo usafishaji damu ifikapo mwaka 2025,” alibainisha.
Dk. Gwajima alisema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa, asilimia 10 ya watu duniani wameathiriwa na ugonjwa sugu wa figo.
Alisema hapa nchini takwimu zinaonyesha kuwa, Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa sugu wa figo kati ya 4,800 hadi 5,200 ambao wanahitaji huduma ya kusafisha damu au kupandikizwa figo.
“Kati ya hao wagonjwa 1000 wanapata huduma ya usafishaji wa damu kwa sasa. Hadi kufikia Novemba, 2020 jumla ya wagonjwa 316 wamepandikizwa figo katika hospitali mbalimbali.
“Mathalani, hapa nchini jumla ya wagojwa 78 wamepandikiwa Figo na Madaktari wazawa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (62) na Hospital ya Benjamin Mkapa (16) na waliobaki wamepandikizwa nchini India,” alisema.
Alibainisha kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Ishi Salama, na Ugonjwa wa Figo”. Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha ushirikishwaji wa mgonjwa wa figo, familia, jamii na marafiki wanaowahudumia waathirika wa ugonjwa sugu wa Figo kuhusu tiba na afya yake ili aweze kuishi salama na ugonjwa wa Figo.
Alisema kiashiria vikuu vya ugonjwa wa Figo ni pamoja na, Shinikizo la juu la damu au ‘Hypertension’, Kisukari au ‘Diabetes’ na Maambukizi ya mara kwa mara ya mfumo wa mkojo au ‘recurrent UTI’.
Alisema kinga ya ugonjwa sugu wa figo ni kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, kula lishe bora na kamili, kunywa angalau lita moja na nusu ya maji kwa siku, usafi wa mwili, kutokuvuta sigara au kunywa pombe kupita kiasi pamoja na kudhibiti shinikizo la juu la damu, kisukari na maambukizi ya mara kwa mara ya mfumo wa mkojo.
“Natoa rai kwa wananchi kuzingatia kanuni za afya ikiwemo kufanya uchunguzi wa afya ‘health checkup’ angalau mara moja kwa mwaka kwenye Kituo cha Afya kilicho karibu na pindi utakapogundulika kuwa na dalili za ugonjwa wa Figo uanze matibabu mapema,” alisema.