Baadhi ya wenyeviti wa mitaa na watendaji wakiwa kwenye kikao kilichoitishwa na mbunge wa Jimbo la mafinga mjini Cosato Chumi
Picha na Denis mlowe
…………………………………………………………
NA DENIS MLOWE, MUFINDI
MBUNGE wa jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi ameagiza wenyeviti wa mitaa, watendaji wa kata na vijiji kusimamia uanzishaji wa benki za matofali kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu kutekeleza agizo la mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi.
Chumi alitoa agizo hilo wakati wa kikao cha kazi jimbo la Mafinga mjini na kuhusisha Wenyeviti wa mitaa na Watendaji wa Halmashauri ya mji wa Mafinga kilichoandaliwa na mbunge huyo na kusema kuwa kuwa na benki ya tofauli itawajenge heshima kwa wananchi na serikali kwa ujumla.
Alisema kuwa wenyeviti wanatakiwa kuhamasisha wananchi kusaidiana katika kuanzisha benki ya tofali kwani itasadia sana kupunguza baadhi ya gharaka kwenye uanzishwaji wa madarasa au ukarabati wa shule mbalimbali katika jimbo hilo.
Alisema kutokana na uchakavu wa majengo mengi ya shule za msingi na nyumba za walimu, kuna haja ya kuweka mkakati wa kuanzisha benki za tofali ili kuendelea kuboresha vyumba vya madarasa na nyumba za walimu hata ukiomba msaada kwa serikali na kuwaambia kwamba kuna matofali inakuwa rahisi zaidi kusaidika.
“Niendelee kusisitiza kila mtaa, kijiji na kata kuwa na benki ya matofali ili kuwezesha ujenzi wa majengo mbalimbali pindi yanapohitajika,” alisema
Alisema kuwa ushirikiano kati ya wananchi na wenyeviti wa mitaa watendaji ni msingi imara katika kuleta maendeleo na kumsaidia Rais John Magufuli katika kurahisisha huduma bora kwa wananchi na kuhakikisha maendeleo yanawafikia kwa urahisi.
Aliongeza kuwa mwenyekiti na mtendaji wa kijiji wakisikilizana na wananchi watahamasika na kushiriki katika shughuli za kujiletea maendeleo na kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jimbo la Mafinga mjini.
Aidha alisema kuwa kama kiongozi wa sehemu husika unapokaa mahali usiangalie sana historia angalia utaacha kumbukumbu gani kwa jamii husika kwani kama historia utaona ipo tu lakini umeacha kumbukumbu gani kwa jamii hiyo.
Alisema kuwa jamii inahitaji sana watu wenye maono kubwa katika eneo unalofanyia kazi na hata thawabu kwa MUNGU inaongezeka kwa mambo mazuri uliyoifanyia jamii na maisha ya kawaida unabarikiwa kutokana na uliyowatendea watu.
Alisema kuwa wakati mwingine ni bora wananchi wakuone mkali lakini jambo ambalo unalisimamia lina manufaa kwao na kwa vizazi vijavyo kwani siku itafika kila mwananchi atakupongeza na kuona faida ya jambo ambalo umelisimamia kwa nguvu zote.
Chumi ambaye ni amekuwa jirani na wananchi wake alisema kuwa kwa upande wao wanapanga mipango ya maendeleo kwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri lakini utekelezaji wake unawategemea zaidi wenyeviti na watendaji hivyo ni muhimu kushirikiana kufanikisha malengo hayo.
Alisema kuwa utekelezaji wa ilani ya chama unawategemea wao hivyo muhimu kuendelea na mshikamano ambao upo na kuwahamasisha zaidi wananchi kujitolea nguvu kazi katika kuboresha sekta ya elimu katika miundo mbinu ya majengo.