Wafanyakazi wa Benki ya NMB wakifurahia uzinduzi wa MastaBata Isiyo Kikawaida.
***************************************
Benki ya NMB imezindua kampeni kabambe ya kufunga mwaka inayolenga kuchagiza matumizi ya kadi za NMB Mastercard na QR miongoni mwa wateja wake ambapo zawadi mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 zitatolewa kwa washindi.
Promosheni hiyo inayojulikana kama MastaBata Isiyo Kikawaida ilizinduliwa rasmi leo jijini Dar es Salaam na itaendelea kwa muda wa miezi mitatu huku zawadi zikitolewa kila wiki na kila mwezi.
Akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Bw. Filbert Mponzi, alisema zawadi hizo ni pamoja na fedha taslimu TZS 100,000 kila wiki kwa washindi 40.
Katika droo ya kila mwezi, wateja 12 watashinda simujanja aina ya Samsung Galaxy Note20 yenye thamani ya TZS 2,480,000. Zawadi kubwa kwenye shindano hili itakayotolewa mwishoni mwa mwezi Februari mwakani ni fursa kwa washindi 12 na wenza wao kusafiri kwa ajili ya mapumziko Zanzibar, Serengeti na Ngorongoro .
Washindi wa droo ya mwisho watagharamiwa gharama zote ikiwemo malazi ya siku tatu, tiketi ya ndege pamoja na pesa za matumizi na watafikia katuka hoteli yenye hadhi ya nyota 5. Pia Bw. Mponzi alisema Benki ya NMB imeona ni vyema washindi wawe na uhuru wakuchagua aina ya zawadi.
Kwa mfano, washindi wa droo kubwa ya mwisho watapewa nafasi ya kuchagua utalii wa ndani au kuchukua kama mbadala zawadi zifuatazo: TV ya kibabe iliolipiwa DSTV miezi mitatu; Friji ya Milango Miwili; Kompyuta Mpakato; Simujanja (Samsung A70); Water Dispenser na Microwave.
Kwa mujibu wa Bw. Mponzi, kampeni ya MastaBata Sio Kikawaida ipo wazi kwa wateja wote wanaomiliki kadi za NMB Mastercard, pamoja na wateja wote ambao wameomba au wataomba kadi mpya katika kipindi cha promosheni hiyo.
Alisema pamoja na kuhamasisha utumiaji wa kadi ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu, promosheni hiyo pia inatoa fursa ya kipekee kwa wateja wa NMB kufurahia huduma za benki hiyo sambamba na mfumo wa maisha ya kidijitali.
“Kadiri unavyotumia kadi katika manunuzi ya mtandaoni au kufanya malipo kupitia mashine za malipo (POS) katika maduka mbalimbali na maeneo mengine nchini, ndipo unapata nafasi ya kushinda zawadi,” Bw. Mponzi alisema.
“Kutakuwa na droo za kila wiki na kila mwezi. Mteja anatakiwa kufanya miamala yake kupitia kadi ya NMB Mastercard au QR mara nyingi iwezekanavyo kwa kuwa kila unapofanya muamala unaongeza nafasi moja ya kushinda,” aliongeza.
Naye Mkaguzi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Rasuli Masudi alihamasisha wateja na wananchi wengine kujiunga kushiriki kwenye promosheni hiyo kwa kuwa imethibitika kuwa ni halali inazingatia vigezo vyote vya utoaji wa zawadi kwa watakaoshinda.