*********************************
Na Emmanuel J. Shilatu
Watanzania tunaadhimisha miaka 21 tangu kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tukiwa na sura yenye matumaini baada ya kufanikiwa kumpata kiongozi anayemuenzi vyema kwa matendo Mwalimu Nyerere.
Naam! Namzungumzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli ambaye tangu aingie Ikulu Novemba 5, 2015 amejipambanua vyema kimatendo kuwa mrithi sahihi wa fikra, matendo ya Mwalimu Nyerere kwenye nyanja tofauti tofauti.
*ELIMU*
Wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere elimu ilikuwa ya lazima na ikitolewa bure kama ambavyo Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Magufuli ambayo hughalamikia zaidi ya Tsh. Bilioni 23.77 kila mwezi kutoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi mpaka sekondari.
*SERA YA VIWANDA NA KILIMO*
Mwalimu Nyerere sera ya viwanda vidogo vidogo (SIDO) na vya kati kama urafiki, Mwatex nk. Pia Mwalimu Nyerere alianzisha program za kilimo mathalani “Utekelezaji wa siasa ni kilimo” mwaka 1974.
Leo hii tunaona Rais Magufuli kupitia serikali yake kujipambanua ni ya Tanzania ya Viwanda ambapo zaidi ya viwanda 3000 vimejengwa ndani ya miaka 2 tu. Pia amefanikiwa kuzindua Sera ya mradi mkubwa wa kilimo awamu II utakaogusa maisha ya Wakulima wadogo utakaowapatia mikopo nafuu ya kilimo.
*RELI*
Miaka ya 1970 Mwalimu Nyerere alijenga reli ya TAZARA ni kama ambavyo leo hii Rais Magufuli anavyojenga reli ya kisasa ya standard gauge itakayotumia umeme.
*ANGA*
Mwalimu Nyerere alianzisha Shirika la Ndege la Air Tanzania ambalo lilikuja kufa katika awamu zilizofuata. Leo hii Rais Magufuli amefanikiwa kulifufua Shirika la ndege kwa kununua ndege mpaka saba ikiwemo ndege kubwa ya Dreamlinear 787-8.
*UMEME*
Mwalimu Nyerere alikuwa na malengo ya kujenga mradi mkubwa wa umeme wa Stiegler’s Gorge lakini hakufanikiwa. Leo hii tunaona Rais Magufuli akiyaendeleza maono ya Mwalimu Nyerere kwa kuanza ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge ambao utatuwezesha Watanzania kuwa na umeme wa uhakiki na nafuu zaidi. Raha iliyoje!
*FALSAFA YA KAZI*
Wakati tunapata Uhuru Mwalimu Nyerere alisema uhuru maana yake ni kazi. Mwaka 1976 aliandika kitabu “Kila Mtu Afanye Kazi” akiendelea kusisitiza Watu wafanye kazi.
Leo hii Rais Magufuli naye amekuja na falsafa ile ile ya kuwataka Watanzania Wafanye kazi kujipatia kipato inayojulikana kama “Hapa Kazi Tu”.
*UDHIBITI WA MADINI*
Mwalimu Nyerere alifanya zoezi la utambuzi wa maeneo yenye madini na kutokuruhusu uchimbaji wa madini. Leo hii tunaona Rais Magufuli akiishi kivitendo kwa kufumua mikataba ya madini na kudhibiti uchimbaji na usafirishaji kiholela wa madini.
*UMASKINI*
Mwalimu Nyerere alipambana vilivyo na adui umaskini kupitia kilimo, viwanda, reli na anga. Ni kama ambavyo leo hii Rais Magufuli anavyopambana na umaskini kupitia kilimo, ujenzi wa reli ya kisasa, ununuzi wa ndege, udhibiti wa mfumuko wa bei na udhibiti wa madini yawanufaishe Watanzania. Anapita njia zile zile za Mwalimu.
*RUSHWA NA UFISADI*
Mwalimu Nyerere alikuwa mkali kabisa dhidi ya rushwa na ufisadi ambapo kipindi cha utawala wake aliyekutwa na hatia ya rushwa alikwenda jela miaka miwili pamoja na kuchapwa viboko 24. Leo hii tunaona mapambano makali dhidi ya rushwa na ufisadi ambapo “Mapapa” wa rushwa wamepandishwa kizimbani tofauti na vipindi vya nyuma walikuwa hawakamatiki.
*KUSIMAMIA MISINGI YA KITAIFA*
Mwalimu Nyerere alijenga umoja wa kitaifa pasipo ubaguzi, aliwahimiza viongozi kuwa karibu na Wananchi kwa kutatua kero za Wanyonge. Ni njia hiyo hiyo anayoitembelea Rais Magufuli leo hii katika uongozi wake.
*KUHAMIA DODOMA*
Wazo la Serikali kuhamia kwenye makao makuu ya nchi mkoani Dodoma liliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere mwaka 1973 lakini lilishindwa kutekelezwa katika awamu zote. Si awamu ya kwanza, wala ya pili, ama ya Tatu au ya nne bali limeweza kufanikiwa kwenye utawala wa Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli. Leo hii karibia Serikali yote imehamia Dodoma. Wizara, taasisi na idara za Serikali, Waziri Mkuu wameshahamia Dodoma. Mwishoni mwa mwaka jana Rais Magufuli naye alihamia Dodoma. Iliasisiwa na Mwalimu Nyerere, ikahaidiwa kwenye ilani ya uchaguzi, imekuja kutekelezwa vyema na Rais Magufuli
Rais Magufuli ameonyesha njia sahihi ya kivitendo ya namna bora ya kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Wajibu wetu sisi Watanzania ni kuendelea kushikamana na kumuunga mkono Rais Magufuli kwenye kila hatua kwani ameonyesha ni Kiongozi aliyejitoa kwa maslahi ya Watanzania.