……………………………………………………………………………………
Ni headline kutokea Mkoani Mbeya ambapo leo October 11, 2020 Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dr. Tulia Ackson ameendelea na ziara zake za kampeni kuelekea Uchaguzi mkuu wa October 28, 2020 ambapo leo alikuwa katika kata ya Uyole Jijini humo akiwaeleza Wananchi sababu za kukichagua chama chake ili kujipatia maendeleo ya kasi zaidi.
“Safari hii Mbeya mjini propaganda zilizoganda tunasukuma nje, kama mtu hakufanya kazi kwa miaka kumi safari hii chagueni CCM mjionee mafanikio ya haraka, CCM tumejipanga kwa ajili ya maendeleo hapa Mbeya mjini na leo nitawaeleza machache tu ambayo tumekwishayafanya na tutayafanya zaidi endapo mtatuchagua kuwatumikia”- Dr. Tulia Ackson
“Tega sikio mwana-Uyole nikueleze kwamba nikianza kwa hapa shule yetu ya msingi Uyole mimi Mbunge wenu wa kujiongeza nimeshapeleka pale madawati hamsini ambayo ni zaidi ya Shilingi milioni nne na laki tano, tukisema safari hii Mbeya mjini tunachagua Mbunge wa kujiongeza basi mjue huko ndio kujiongeza. Sikuwa na mfuko wa Jimbo lakini mmeyaona niliyoyafanya”- Dr. Tulia Ackson
“Mtaa wetu wa Hasanga hapo Shule ya Hasanga changamoto zao nazijua na nikisema nitazishughulikia ni kwasababu kazi imeanza, kwahiyo hata shule ya msingi Kilimo tutaifikia kwasababu sisi ni watu wa kazi sio manenomaneno. Shule yetu ya Sekondari Pankumbi tumeshapeleka pale mabati 100 ambayo gharama zake ni karibu Milion mbili na laki saba, tumepeleka mifuko 100 ya cement sasa ndugu zangu nawaeleza kwamba tupo vizuri na tumejipanga”- Dr. Tulia Ackson
“Twende kwenye eneo la afya, hapa Uyole tunatumia kituo cha afya Igawilo na sasa kile kituo cha afya kinaenda kuwa Hospitali ya Wilaya na tayari Rais Magufuli ameshapeleka pale Milion miatano na hamsini, pamoja na Rais Magufuli kupeleka fedha hizo mimi Mbunge wenu wa kujiongeza pia nimeshapeleka pale mashuka na kitanda kwa ajili ya kujifungulia Mama zetu. Huu ni muda wa hesabu na asiyefanya kazi tunasukuma nje”- Dr. Tulia Ackson
“Kwenye Ilani yetu ya CCM 2020-2025 kwenye ukurasa wa 66 inaeleza kwamba barabara yetu hapa Mbeya mjini kutoka hapa Uyole hadi Tunduma KM 104 zinajengwa njia nne na pia itaungana na barabara ya kuelekea hadi Igawa. Kwahiyo asitudanganye mtu kwamba tutakwama kwenye foleni, foleni haitakuwepo tena ukimchagua John Pombe Magufuli na Tulia Ackson. Mimi naitwa Mama wa Connection sasa kwa urahisi tu ili haya yote myapate mkumbuke jambo moja tu mnapaelekea kwenye kupiga kura mnataja jina la TULIA na MAGUFULI bila kusahau Madiwani wote wa CCM”-Dr. Tulia Ackson