Home Mchanganyiko UDHALILISHAJI WA KIJINSIA KWA MTOTO WA KIKE BADO CHANGAMOTO ZANZIBAR

UDHALILISHAJI WA KIJINSIA KWA MTOTO WA KIKE BADO CHANGAMOTO ZANZIBAR

0
Mwenyekiti wa Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar Jaji Mshibe Ali Bakari akizungumza akieleza juu ya umuhimu wa jamii kubadilika na kupinga udhalilishaji dhidi ya watoto.
Wanafunzi wakionesha igizo ambalo lilienga mjomba kumbaka mtoto wa dada yake na kumpatia ujauzito huku wakionesha uhalisi kuwa matendo ya udhalilishaji kwenye jamii fufanywa na watu wa karibu.
Miongoni mwa watoto waliohudhuria katika hafla hio iliofanyika katika kituo cha kulelea watoto SOS mjini Unguja.
Picha ya pamoja kwa washiriki  waliohudhuria katika hafla hio iliolenga kumlinda mtoto wa kike dhidi ya matukio ya udhalilishaji.
……………………………………………………………………
Wakati leo Dunia  ikiadhimisha siku ya mtoto wa kike kila ifikapo tarehe 11 ya mwezi Oktoba inaelezwa kuwa visiwani Zanzibar jumla kesi 761  za udhalilishaji zimeripotiwa katika vituo mbali mbali vya polisi kutoka mwezi Januari mwaka 2019 hadi ogast 2020.
Hayo yamelezwa na Meneja sera na utetezi Tamwa-Zanzibar Salma Amir Lusangi katika maadhimisho ya siku hio kwa upande wa asasi za kiraia visiwani hapa .
Alisema kesi hizo ni aina mbali mbali za udhalilishaji wa kimaumbile ambapo jumla ya watoto 649 wameharibiwa sehemu za mbele za maumbile yao na watoto 147 wamelawitiwa na kufanywa kinyume na maumbile.
Alisema  kuwa licha ya idadi kubwa ya kesi zilizoripotiwa kwa watoto waliofanyiwa matendo hayo  katika sehemu za mbele za maumbile  lakini ni kesi nne tu ndio zilizopatikana na hatia na hatimae waliofanya kupewa adhabu ya kifungo gerezani na kesi 370 bado zipo katika vituo mbali mbali vya polisi hadi sasa zikiendelea na uchunguzi tangu mwaka 2019.
Wakati hayo yakijiri pia alisema kesi 123 zipo Mahakamani na kesi 80 zimefungwa wakati  kesi 48 zipo katika ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka (DPP) huku  kesi 16 washtakiwa wameachiwa huru.
Akitolea ufafanuzi kuhusu watoto waliolawitiwa kinyume na maumbile alisema kuna kesi 147 na hadi sasa ni mtuhumiwa mmoja pekee ndio aliepatikana na hatia na kisha kufungwa gerezani wakati kesi 93 hadi leo hii zipo katika vituo mbali mbali vya polisi  Unguja na Pemba na kesi 15 zimefungwa huku  kesi 6 bado zipo  ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka (DPP) zikisubiri kufikishwa Mahakamani.
Licha ya uwepo wa hali hio pia  Meneja huyo aliesema katika uchunguzi uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tamwa-Zanzibar  umebaini kuwa uwepo wa watoto 88 ambao wamepewa mimba wakiwa na umri mdogo na kukatishwa kabisa masomo yao kutoka mwaka 2017-2019.
Sambamba na hayo alisema pia katika kipindi cha miaka mitatu kutoka mwaka 2017 hadi 2019  takwimu kutoka wizara ya elimu zinaonesha kuwa watoto 50 wamelazimisha kufunga ndoa wakiwa na umri mdogo kinyume na maelekezo ya watalamu wa afya ambao mara nyingi hushauri mtoto kuanza kuolewa akiwa na zaidi ya miaka 18.
Alieleza kuwa kuna  dalili mbali mbali ambazo zinaonesha uwepo idadi kubwa zaidi wa matukio ya aina hio lakini baadhi ya wanajamii wameamua kuyaficha na kutotolea taarifa kutokana kwa sababu wanazozijua wao ikiwemo muhali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kijiji cha SOS Asha Salim Ali  alisema kuna watoto wengi bado Zanzibar wamekua wakikabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo bado hazijpatiwa ufumbuzi.
Hata hivyo alisema bado Zanzibar inahitaji mabadiliko ya kisheria ambazo zitalenga kuwalinda watoto na kadhia mbali mbali zinazowasibu.
Alieleza kuwa bado wananchi walio wengi wakiwemo watoto wenyewe wanavilio vya kila siku ambavyo hadi leo hii havijapatiwa ufumbuzi ndio maana anaamini matendo ya udhalilishaji kwa watoto yanaendelea kushamiri siku hadi siku.
Akisoma risala kwa niaba ya watoto wenzake Mwanafunzo kutoka shule ya kajificheni Salamuu Mohamed alisema watoto wenzao wengi wamekua wakikabiliwa na changamoto za kufanyiwa matendo ya ubakaji na na wengine kulawitiwa kinyume na maumbile na kuwafanya wengi wao kukosa furaha sambamba na kunyanyapaliwa wanapoamua kurudi tena shuleni kuendelea na masomo yao jambo ambali alisema wengine hua sababu ya kuacha kabisa kusoma.
 
Pia alisema suala la ndoa za mapema zimekua zikiwafanya baadhi ya wenzao kushindwa kutimiza ndoto zao za kielimu na badala yake hujikuta wakiwa mama wa familia tena wenye umri mdogo katika jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar Jaji Mshibe Ali Bakari alisema licha ya jitihada mbali mbali zinazofanywa na taasisi bado kuna tatizo katika jamii ambayo inaonekana haijawa na mwamko wa kudhibiti matendo hayo na ndio maana kumekuepo na idadi kubwa ya ndoa za umri mdogo sambamba na matendo mengine.
Alisema kwa mitazamo hio ipo haja kwa ofisi yake kufanya kazi ipasavyo ikiwemo kutoa elimu kila kijiji Unguja na Pemba ili jamii iweze kufahamu madhara hayo kwa watoto.
Aidha Mwenyekiti huyo alisema  jamii na wanaharakati wanapaswa kufahamu kuwafikisha watoto Mahakamani ama vituo vya polisi ni kuchelewa kwa kuwa mtoto aliebakwa ama kulawitiwa hawezi tena kurudi hali ya kawaida hata kama aliefanya hivyo atafungwa maisha gerezeani.
‘’Kama mtoto kadhalilishwa hata sheria ikichukua mkondo wake bado maumivu ya mtoto yatabaki milele dawa ni kuhakikisha watoto hawafanyiwei matendo haya katika jamii zetu’’aliongezea.
Alieleza kuwa  jambo la kufanya ni kuhakikisha matendo hayo hayafanyiki kwa njia yoyote hile na sio kukadhania kuwapeleka vituo vya polisi wafanyaji wakiamini kuwa ndio suluhisho lake.
Wakati hayo yakijiri Mwenyekiti huyo aliitaka jamii kufahamu kuwa  sheria ina mlolongo mkubwa mpaka mtu kutiwa hatiani na ndio maana zipo kesi nyingi ambazo huondolewa Mahakamani kwa kuwa waliofanyiwa matendo hayo hufunga ndoa na kutokua tayari kumtolea ushahidi mume wake wa ndoa.
Alisema ni lazima jamii ifahamu kuwa inachokifanya Mahakama ni kutoa dhabu kwa alietenda kosa lakini haina uwezo wa kumrudisha katika hali yake ya kawaida mtoto alielawitiwa ama kubakwa.