Mkuu wa wilaya ya Longido akizungumza kwenye halfa ya kukabidhi hundi ya shilingi 150 kwa vikundi 38 katika wilaya ya longido jana.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido Dkt Jumma Mhina akizungumza katika hafla ya kukabidhi Hundi ya Shilingi 150 kwa Vikundi 38 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu
Kulia Mkuu wa Wilaya ya Longido Frank Mwaisumbe akimkabidhi Hundi ya Shilingi 150 Bi.Grace Mgase ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Longido
Kinamama wakiwa wameshikilia Hundi ya Shilingi Milioni 150
************************************
Na Pamela Mollel,Longido
Halmashauri ya Wilaya ya Longido Mkoani Arusha imetoa Mkopo wa shilingi Milioni 150 kwa vikundi 38 vya Wanawake,Vijana na Watu wenye Ulemavu bila riba, kwa lengo la kuwainua kiuchumi.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi Hundi kwa vikundi hivyo jana,Mkuu wa Wilaya ya longido Frank Mwaisumbe alisema kuwa mikopo hiyo itasaidia kuchochea kasi ya maendeleo Wilayani hapo na kuwaasa kutumia vyema mikopo hiyo pamoja na urejeshwaji mzuri ili vikundi vingine viweze kunufaika
Mwaisumbe alipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi,huku akiwahamasisha jamii hiyo ya kifugaji kuanzisha Viwanda vidogovidogo vitakavyowasaidia kukuza uchumi wao
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ya Longido Dkt Jumma Mhina alisema kuwa vikundi vilivyopo katika kata zote 18 zimenufaika na mkopo huo wa asilimia kumi, na kwa Sasa wanaendelea kutoa elimu kwa vikundi hivyo ya namna bora watakavyo tumia mikopo hiyo kwa ufasaha ili waweze kunufaika
“Sambamba na utoaji wa mikopo vikundi hupewa semina maalumu na kazi hiyo hufanywa na kamati ya mikopo kwa kuwaelimisha na kuwapa mbinu bora za kufanya ujasiriamali”alisema Dkt Mhina
Dkt Mhina alisema Wilaya hiyo kwa asilimia kubwa ni Wafugaji hivyo vikundi vingi vinategemia kunenepesha Mifugo na tayari wameshaanzisha Kiwanda cha Nyama ambacho ni fursa kwao
Naye Afisa maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Longido Bi.Grace Mgase alisema kuwa muamko wa ukopaji ni mzuri kutokana na kinamama, Vijana na watu wenye Ulemavu kujitokeza kwa wingi ukilinganisha na kipindi cha nyuma
Bi.Mgase anashukuru Uongozi wa Halmashauri hiyo kwa kumpa ushirikiano mkubwa pindi anapohitaji fedha hizo
Wanufaika wa mikopo hiyo Nakepo Laizer na Mwalimu Mathayo Mopia ambaye ni Katibu wa Kikundi cha Mwangaza wa Neema kwa watu wenye Ulemavu wanashukuru serikali kwa kuendelea kuwawezesha Wananchi wake
Serikali hutenga asilimia 10 ya mikopo,kwa makundi ya Wanawake asilimia 4,Vijana asilimia 4 na watu wenye Ulemavu asilimia 2.