Katibu wa Itikadi na Uenezi (CCM) Ndugu Hupmhrey Polepole akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu wa Itikadi na Uenezi (CCM) Ndugu Hupmhrey Polepole wakati akizungumza nao leo katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakifuatilia kilichokuwa kikizungumza na Katibu wa Itikadi na Uenezi (CCM) Ndugu Hupmhrey Polepole.
…………………………………………..
Katibu wa Itikadi na Uenezi (CCM) Ndugu Hupmhrey Polepole amekishutumu chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na kusema vipi viongozi wa Chama hicho wanamuacha mgombea wao anazungumza vitu vya uongo wakati takwimu zipo na nyaraka zipo kama ambavyo zinaeleza kila kitu.
Polepole ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma leo akisema kama Tundu Lissu hajui mambo atuulize tumueleze lakini si kupita na kusema uongo.
“Nadhani huyu mtu kuna mahali hapako sawa kutokana na matatizo aliyokutana nayo, sitaki kunasibisha matatizo aliyoyapata na uwezo wake mdogo wa kumbukumbu,” amesema Polepole.
Polepole ametolea mfano wa umuhimu wa kuanzisha mashirika ya ndege na uamuzi mgumu wa kununua ndege , akitolea mfano kwa kumtaja mtawala wa Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Mfalme Mohamed Bin Rashid Al Maktoum ambapo mwaka 2001 alifanya uamuzi mgumu wa kununua ndege 56 kwa wakati mmoja.
Amesema Al Maktoum alipata kusema hakuwahi kufanya uamuzi mgumu katika maisha yake kama huo, lakini leo tunaona shirika la ndege linaloongoza kwa ukubwa duniani ni Emirates. Hivyo, hata Rais Magufuli kwa uamuzi wa kununua ndege wapo wanaombeza lakini watakuja kumkumbuka,” amesema Polepole.
Akizungumzia kuhuishwa kwa Shirika la Ndege (ATCL), ambapo alikumbusha kuwa hadi mwaka 2015/16 shirika hilo lilikuwa hoi “Mpechempeche” kifedha, lilikuwa linatengeneza hasara huku likiwa na ndege moja tu tena mbovu na ya kukodi. Lakini ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano zilinunuliwa ndege 11 ambapo hadi sasa ndege nane zimeshawasili.
Kingine alichogusia ni namna Lissu alivyosema ndege zilinunuliwa bila kuidhinishwa katika bajeti ya taifa, amemkumbusha katika mazungumzo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hansard zinaonyesha kati ya Juni 2016 hadi Juni 2018 inaonyesha namna wabunge walivyokuwa wakijadiliana juu ya kununuliwa ndege na fedha zikatengwa.
Polepole amesema wapo wanaotumia kampeni za mwaka huu kuzungumza uongo na kuzua tafrani kuhusu viwanja vya ndege , kwa sababu suala la viwanja vya ndege si la eneo moja au la kumpelekea mtu bali la wananchi na kuleta maendeleo.
Ameitaja baadhi ya mikoa ambayo kuna viwanja vinavyokarabatiwa na vingine vinajengwa vipya ni pamoja na Dodoma, Singida, Mpanda, Chato, Tabora, Mtwara, Musoma pamoja na Shinyanga.
Polepole amesema anashangazwa na Tundu Lissu anaposema uwanja wa ndege wa Mpanda hautumiki, kitu ambacho si cha kweli kwa hadi juzi ndege ilitua kwa kuwa uwanja huo unatumiwa na watalii wanaokwenda Hifadhi ya Taifa ya Katavi.
Ameongeza kuwa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaoendelea kwa sasa kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora na baadaye hadi Mwanza kumefanyika upembuzi yakinifu kuihuisha reli ya zamani ikiwemo kuiongezea uwezo reli ya kati na kuifufua reli ya Kaskazini.
“Reli ya kati tuliiongezea ratili ili iweze kubeba mizigo mizito na abiria wengi zaidi pamoja na kuiongezea kasi, ilikuwa na ratili 45 imepanda hadi 60. Itakuwa na uwezo wa kubeba mzigo mkubwa pamoja na kuwa na kasi inayofikia kilomita 70 kwa saa,” amesema Polepole.