Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua moja ya aina bora ya mbuzi wanaopatikana Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Kituo cha West Kilimanjaro.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akichunga kondoo waliopo katika Ranchi ya West Kilimanjaro inayomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na kufurahishwa na afya ya mifugo hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua ng’ombe waliopo katika Ranchi ya West Kilimanjaro inayomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na kufurahishwa na afya ya mifugo hiyo. Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua moja ya aina bora za kondoo wanaopatikana Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Kituo cha West Kilimanjaro.Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Kituo cha West Kilimanjaro.
***********************************
Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya MIfugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kuendelea kufanya tafiti za kisasa zaidi ili sekta ya mifugo iweze kuwa na endelevu.
Akizungumza jana (17.09.2020) katika Ranchi ya West Kilimanjaro iliyopo Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro, kwenye kituo cha TALIRI Prof. Gabriel amesema sayansi na teknolojia inabadilika kwa kasi kubwa hivyo lengo serikali ni kubadilisha wafugaji waingie kwenye ufugaji wa kisayansi kwa kupata ng’ombe na mbuzi bora kwa njia ya kumpandikiza mnyama mimba kwa njia ya mrija.
“Kwa ukanda huu wa kaskazini kituo hiki cha TALIRI ni mkombozi mkubwa sana tunataka tubadilishe familia ya ufugaji tuingine kwenye sayansi.” Amesema Prof. Gabriel
Aidha, akiwa katika ranchi hiyo yenye ukubwa wa hekta 23,000 inayomilikiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) na hekta 5,600 inayomilikiwa na TALIRI, Prof. Gabriel ametoa rai kwa wananchi wanaoishi karibu na miundombinu ya serikali na maeneo yakitafiti wasifikiri maeneo hayo yameachwa kiholela bali ni maeneo muhimu kwani bila tafiti mifugo haiwezi kuendelea.
Katibu mkuu huyo ameutaka pia uongozi wa TALIRI katika ranchi ya West Kilimanjaro kufikiria namna ya kufanya uzalishaji ili mapato ya kituo yaongezeke na kuwa na miundombinu mizuri kwa kutenga eneo la utafiti lakini pia kutenga eneo la uzalishaji.
“Mkiweza kujiweka vizuri katika mapato mtafanya kazi vizuri na muone kuwa na mradi mkakati kwa ajili ya kuongeza uzalishaji kuhusu mitaji kuna Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), mkiandika andiko zuri fedha zitapatikana na mtatengeneza mapato makubwa muweze kutoa gawio kubwa serikalini.” Amefafanua Prof. Gabriel.
Kuhusu NARCO, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema serikali imefanya kazi nzuri kwa kuhakikisha uwepo wa viwanda vingi nchini, vikiwemo vya nyama hivyo kampuni hiyo inatakiwa ijipambanue kwa kuwa na mifugo mingi maana hitaji la nyama na ngozi kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali litaongezeka.
“Ndani ya kampuni ya NARCO, ranchi ya West Kilimanjaro imekaa kimkakati mitaji ia inapatikana kirahisi tuko karibu na TADB, kwa hiyo NARCO watafanya mipango ya uwepo miradi ya kimkakati ikiwepo ya kuendeleza ufugaji wa kisasa kwa kuongeza idadi ya mifugo katika ranchi hii.” Amefafanua Prof. Gabriel.
Ameongeza kuwa ranchi hiyo ipo katika eneo zuri kwa kuwa karibu na barabara, uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) pamoja na kituo cha treni hivyo njia za kiusafiri zina faida kubwa, hali kadhalika uwepo wa hali nzuri ya hewa yenye ubaridi ambayo ni nzuri kwa ukuaji wa mifugo hivyo kuutaka uongozi wa NARCO kuhakikisha ranchi hiyo inakuwa na faida kubwa kwa taifa.
Amezitaka pia TALIRI na NARCO katika ranchi ya West Kilimanjaro kuwa na mahusiano mazuri na wananchi wanaoishi pembezoni mwa ranchi hiyo pamoja kushiriki katika kutoa michango mbalimbali ya kijamii.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kituo cha West Kilimanjaro, kituo hicho kina mbuzi 254, kondoo 303 na ng’ombe 53 ambao wanatumika katika miradi mbalimbali ya kuhifadhi, kuboresha na matumizi endelevu ya koo za mbuzi na kondoo wa kienyeji wanaopatikana hapa nchini, huku Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Ranchi ya West Kiliamnjaro ikiwa na ng’ombe 660, kondoo 824 na farasi watano.
Pia, NARCO imepata mafanikio mbalimbali yakiwemo ya kuvuna malisho ya mifugo kwa ajili ya mifugo ya ranchi hiyo na kuwauzia majirani, kutenga vitalu kwa ajili ya wafugaji katika vijiji vinavyozunguka ranchi kwa ajili ya ufugaji wa kibiashara na kisasa zaidi.