*************************************
Kampuni ya Tanzania Breweries Public Limited Company(TBL Plc) imezindua kampeni ya kuhamasisha utumiaji wa vinywaji vyenye kilevi kistaarabu inayojulikana kama ‘Pombe sio Chai, Kunywa Kistaarabu’.
Kampeni hii imelenga kubadili tabia za watumiaji wa bidhaa za pombe kutambua tofauti ya unywaji wa kupita kiasi na unywaji wa kistaarabu na itafanyika kwa kuelimisha faida za unywaji wa kistaarabu kupitia njia mbalimbali zikiwemo redio,magazeti,njia za mitandao ya kijamii ya kidigitali na kampeni za moja kwa moja kwa wateja.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL Plc, Philip Redman alisema “Tukiwa kampuni inayoongoza kwa kutengeneza vinywaji nchini, tunaamini ni jukumu letu pia kuhamasisha watumiaji wa bidhaa zetu nchini Tanzania kubadilisha mienendo yao kwa kuzitumia kistaarabu. Mkakati wetu wa kutoa elimu hii umelenga kubadili tabia za watumiaji katika jamii na kufanikisha sera ya biashara yetu ya kuleta mabadiliko chanya kwa kujenga jamii inayotumia vinywaji kistaarabu’’.
Aliongeza kusema kuwa kampeni ya ‘Pombe sio Chai, Kunywa Kistaarabu’ itajikita kwenye masuala ya athari za matumizi ya pombe kupita kiasi kwa watu wazima, matumizi ya pombe kwa wenye umri mdogo na makundi maalumu kwenye jamii kama wajawazito, matumizi ya vinywaji ambayo yanaweza kuleta madhara kwa watu wengine kama kuendesha vyombo vya moto ukiwa umelewa.
“Tunaamini kuwa matumizi ya bia yawe na matokeo chanya na ndio maana tunahimiza watumiaji na wateja kwa ujumla kunywa kistaarabu’, aliongeza kusema Redman.
Kwa kipindi cha muda mrefu kampuni ya TBL imekuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya unywaji wa kistaarabu katika makundi mbalimbali ya jamii. Dira ya kampuni ni kuendesha kampeni zenye kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii katika maeneo inakofanyia biashara zake.