Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. John Pombe Magufuli akiwahutubia wananchi kwenye uwanja wa Mkendo mjini Musoma mkoani Mara katika mkutano mkubwa wa Kampeni leo Jumamosi Septemba 5, 2020. Ili kuomba kuchaguliwa katika uchaguzi Mkuu wa Rais ,Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Jumatano Oktoba 28,2020 nchini nzima.
Mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mama Maria Nyerere akizungumza na wananchi na kumuombea kura Rais Dk. John Pombe Magufuli katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Mkendo mjini Musoma.
Mgombea Ubunge jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo akimuombea kura Rais Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Mkendo mjini Musoma leo.
Umati wa Wananchi waliohudhuria katika mkutano huo.
Na John Bukuku, Musoma
Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. John Pombe Magufuli amesema Katika utawala wake Mungu akimjaalia yale yote aliyoyaahidi baba wa taifa atayatimiza kwa kasi sana na pia kuuenzi mkoa huo alioazaliwa baba wa taifa.
Ili kumuenzi baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere nitanimiza yote aliyoahidi Baba wa Taifa ambaye ni muasisi wa taifa hili lenye amani na utulivu kazi ambayo Mwalimu Nyerere aliifanya kwa uadilifu na uaminifu mkubwa kwa watanzania.
Amemshukuru Mama Maria Nyerere kwa kumuombea kura kwa wananchi wa Mkoa wa Mara baada ya kufika katika Mkoa huo kwa ajili ya kampeni.
“Asante sana Mama Maria kwa kuja kuniombea kura, sina cha kusema zaidi ya Asante Mama kwa kuendelea kukienzi Chama cha Mumeo, lakini wewe ni muwazi, hata Mwanao (Makongoro) alipozungumza hadi kula muda wako uliona vile vikaratasi na ukamwambia umekula muda wangu”. Amesema Rais Dkt.Magufuli.
Rais Magufuli amesema hayo katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Mkendo mjini Musoma leo na kuwaomba wananchi wa mkoa wa Mara kumpigia kura katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 28, 2020 siku ya jumatano.
Amesema wakati akiingia madarakani mwaka 2015 upatikanaji maji ulikuwa asilimia 44.4 mkoani humo na sasa umefikia asilimia 64.9, ambapo ameahidi kuwa akipewa miaka mitano mingine itafikia asilimia 100.
“Shilingi Bil 49 zimetengwa kwa ajili ya uwanja wa ndege wa lami. Haiwezekani Mama Maria akitaka kwenda Dar es Salaam asafiri kwa gari hadi Mwanza.” Amesema Dk. Magufuli.
Katika suala la barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami ni kilomita 283k na zilizojengwa kwa changarawe ni kilomita 1147 pamoja na madaraja sita.
Miradi 38 ya maji imetekelezwa kwa gharama ya Sh Bil 68.4 ambapo kati ya hiyo miradi 17 imeshakamilika na wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama.
Katika kushughulikia suala la umeme vijijini Rais Dk.Magufuli amefafanua kuwa serikali imepeleka umeme katika vijiji 411 kati ya vijiji 458, vimebaki vijiji 47 pekee kwa gharama ya Sh Bil 105.4 hivi vilivyobaki haviwezi kutushinda kukamilisha tupeni miaka mitano mingine tukamalize kazi.
Awali mgombea Ubunge jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo amesema mkoa wa Mara una utajiri wa rasilimali za madini ambazo Rais Dk John Pombe Magufuli alilazimika kusimamia sekta hiyo kwa kuhakikisha vijana wananufaika nayo kwa kuwaondolea baadhi ya kodi na kuwapa leseni 675 wachimbaji wadogo pamoja na kujenga masoko ya madini katika migodi ya Musoma, Nyamongo na Tarime.
Muhongo amesema Rais Magufuli ametekeleza vyema suala la ajira kwa vijana na ajira zitapatikana kuendana na ukuaji wa uchumi, kwa kuwa uchumi wetu unakua kwa asilimia saba, ilani hii ya uchaguzi mkuu mwaka 2020 ukiisoma inasema ongezeko la uchumi ifikie asilimia nane na watalaam wa uchumi duniani kote wanasema ukitaka kuondoa umasikini lazima uchumi uende juu kwa asilimia nane.
Uchumi wetu, kwa miaka mingi umekuwa ukikua kati ya asilimia tano mpaka asilimia saba, ongezeko la Watanzania ni watu milioni 59.7 na thamani ya uchumi wetu ni Dola za Marekani Bilioni 62.2.
Profesa Sospeter amesema duniani viongozi wa nchi na serikali wanaopendwa ni wale wanaokuza uchumi hii ndiyo sababu inayonifanya nimuombee kura Dk. Magufuli kutokana na mambo makubwa aliyowafanyia wananchi wa Mkoa wa Mara.