*********************************
Na Mwandishi wetu, Babati
Madereva watatu wa malori waliokatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wakishirikiana na polisi wakidaiwa kukwepa ushuru wa mazao, wamelipa faini baada ya kukiri makosa.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari amesema baada ya madereva hao kukiri kosa wamepigwa faini ya shilingi 1,095,250 na kuilipa halmashauri ya wilaya hiyo.
Makungu amesema madereva hao walishirikiana na mtumishi wa halmashauri hiyo Joachim Soka kukwepa ushuru wa mazao ya vitunguu kwenye eneo la Kitichamungu mpakani mwa mkoa wa Kilimanjaro.
Amesema madereva hao kutoka nchi ya jirani walikamatwa na TAKUKURU kwa kushirikiana na polisi wakidaiwa kula njama na mtumishi huyo ili kukwepa ushuru kwa kulipa fedha kidogo kuliko idadi ya magunia waliyoyabeba na kusababisha hasara.
“Baada ya mahojiano na madereva hao wenye magari yenye namba T450 AZP, KCM 411 K na KCU 073 X walieleza kuwa wamekuwa wakishawishiwa na watumishi na kupokea stakabadhi zinazoonyesha wamelipa kiasi cha fedha tofauti na uhalisia,” amesema Makungu.
Amesema baada ya makubaliano hayo madereva hupewa bakshishi kidogo na huku maofisa hao wakibaki na sehemu kubwa ya fedha mikononi mwao.
Amesema kutokana na wao kukiri makosa madereva hao walipigwa faini na kuachwa waendelee na safari kwani vitunguu ni zao linaloweza kuharibika mapema.
“Napenda wamiliki wa malori, madereva na wafanyabiashara wafahamu kuwa zoezi hilo ni endelevu na tutatoa onyo kwamba wakati ujao kwa watakaokamatwa hawatapigwa faini tena kwa sheria za halmashauri bali watashtakiwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi kama ilivyorekebishwa na sheria namba 3/2016,” amesema.
Amesema chini ya sheria hiyo watakaodhibitika kuhujumu uchumi, ambapo adhabu ni kifungo kisichopungua miaka 20 jela pia chombo kilichotumika kusafirisha mazao kinataifishwa.
Amesema kwa upande wa mtumishi wa halmashauri hiyo aliyehusika kwa kuzingatia nukuu ya Jaji Mkuu mhe Profesa Ibrahim Hamis Juma aliyoitoa Juni 17 mwaka huu kuwa utashi wa kisiasa na dhamira anayoonyesha mhe Rais John Magufuli haitoshi bila kila taasisi, kila idara na kila mwananchi kukubali kwa vitendo kuwa sehemu ya vita dhidi ya rushwa.
“Ni dhahiri kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ambaye pia alishirikiana na TAKUKURU katika zoezi zima la ukamatwaji wa malori hayo atachukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya mtumishi huyo kabla ya TAKUKURU haijamchukulia hatua kali.
“Kwa ushirikiano huo itakuwa fundisho kwa watumishi wachache wanaoihujumu halmashauri ya wilaya ya Simanjiro na wote wenye mawazo ya kuhujumu mapato kama ya Soka,” amesema.