Waziri Wa Afya Ummy Mwalimu akioneshwa ramani ya majengo ya Hospitali mpya ya Rufaa ya mkoa wa Geita inayoendelea na ujenzi. Anayemuonesha ni Eng. Gladis Jefta anayesimamia mradi huo. Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Geita Dkt. Shaban Massawe akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipotembelea Ujenzi wa Hospitali hiyo.
**********************************
Na WAJMW-Geita
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo ametembelea Hospitali mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Geita inayoendelea na ujenzi na ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo ambao umefikia asilimia zaidi ya 93 uliogharimu Tsh. Bilioni 15.3.
Waziri Ummy ameitaka Hospitali hiyo kuanza kutoa huduma ndani ya wiki mbili huku akimtaka Mganga Mfawidhi Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Japhet Simeo kuhakikisha vifaa muhimu vya kutoa huduma vinafungwa na kuanza kufanya kazi katika muda huo.
Aidha, Waziri Ummy ameupongeza mkoa wa Geita kwa kuboresha huduma za afya kwa kujenga zahanati katika vijiji 117 vilivyoko mkoani humo.
Hata hivyo, amesifu jitihada zilizowekwa na mkoa katika kuboresha afya ya mama na mtoro ambapo vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 1300 mwaka 2015 mpaka kufikia 311 mwaka 2019, halikadhalika idadi ya akinamama wajawazito kwenda kujifungua katika vituo vya afya imepanda kutoka 40 kati ya wanawake 100 na kufikia 100 kati ya 100 na hali hiyo imetokana na uboreshwaji wa huduma za afya katika mkoa huo na hivyo kupelekea vifo vya wajawazito kutoka 112 mwaka 2015 hadi kufikia vifo 24 mwaka 2020.