Home Biashara Vodacom Tanzania PLC yazindua Duka Kubwa la Kisasa mjini Lindi

Vodacom Tanzania PLC yazindua Duka Kubwa la Kisasa mjini Lindi

0

Mkuu wa wilaya ya  Lindi, Shaibu Ndemanga (katikati) akikata utepe kuzindua duka la kisasa la Vodacom mjini Lindi mwishoni mwa wiki ili kuwafikishia wananchi huduma karibu yao. Kushoto ni Mkuu wa Mauzo wa Vodacom kanda ya Pwani na Dar Es Salaam, Brigita Stephen na Meneja wa Vodacom Lindi,  Omary Kilumanga.

*************************************

Mkuu wa wilaya ya  Lindi,Shaibu Ndemanga amepongeza kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania PLC kwa kuwasogezea huduma mkoani humo na hivyo kuwaondolea adha ya kwenda Mtwara kufuata huduma.

 Alisema kwa muda mrefu wakazi wa Lindi walipokuwa wakihitaji huduma za Vodacom walikuwa walilazimika kwenda Mtwara kupata huduma.

 Mkuu huyo wa wilaya  alisema hayo wakati wa uzinduzi wa duka kubwa la kisasa la kampuni hiyo ya simu mkoani Lindi, lililopo mtaa wa soko kuu mjini Lindi.

 Aliendelea kusema ” kuwapo kwa duka hilo  kutasaidia uimarishaji wa mawasiliano hasa ikizingatiwa kwamba mkoa huo sasa unakwenda kuwa mkoa wa viwanda na shughuli nyingi za kijamii kama elimu na masuala ya bandari ” alisema Ndemanga .

Aliongeza kuwa mkoa huo ukiwa na mpango wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi, ufunguzi wa kituo cha  taasisi ya usafirishaji kwa ajili ya mafunzo ya bahari na pia chuo kikuu huria kunafanya mawasiliano kuwa kitu cha maana na muhimu zaidi.

 Alimaliza kusema “naamini kwamba uamuzi huu wa Vodacom utasukuma maendeleo ya mkoa wetu na niwaombe pia wajikite vijijini ili kubadili masha ya wananchi”. alimaliza kusema Ndemanga

 Naye Mkuu wa Mauzo wa Vodacom kanda ya Dar es salaam na Pwani, Brigita Stephen alisema  kampuni hiyo ya simu yenye wateja zaidi ya milioni 15 sasa imepiga hodi katika mkoa wa Lindi rasmi na kutaka wananchi watumie huduma zao ambazo zina ubora na upekee.

 Alisema “ufunguzi wa duka hilo unafanyika huku tayari  kampuni hiyo ikiwa na maduka madogo 233 na makubwa 100  nchini kote”.

Aliendelea kusema “lengo la kusogeza huduma ni kuhakikisha kwamba Tehama inatumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi  na kufaidi huduma inayotolewa na mtandao huo”. alisema Brigita

Aidha  Brigita amesema kwamba wameimarisha upatikanaji wa mtandao kwa kasi ya 4G.

 Aliwataka wananchi kutumia duka kubwa hilo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali zikiwemo za ununuzi wa simu na kujua bidhaa mbalimbali.