*******************************
Na Mwandishi Wetu,
MAELEZO
DAR ES SALAAM
23.6.2020
SERIKALI ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wakulima na wafanyabiashara na pia kuboresha miundombinu ili kuwezesha upatikanaji wa chakula na masoko ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi katika maeneo yote nchini.
Dhamira hiyo inatokana na ukweli kuwa sekta ya kilimo kuwa mhimili muhimu katika maendeleo ya uchumi wa taifa letu ambapo Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia bei za mwaka 2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka Tsh. trilioni 25.2 mwaka 2015 hadi Tsh. Trilioni 29.5 mwaka 2019.
Aidha sekta imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania huwapatia ajira wananchi kwa asilimia 65.5 na kuchangia malighafi za viwanda kwa asilimia 65 pamoja na kuchangia asilimia 30 ya fedha za kigeni., na kuifanya kuwa sekta muhimu kwa mmaendeleo ya uchumi wa wananchi katika wakati huu tunapojidhatiti kufikia uchumi wa viwanda na umuhimu wa malighafi za mazao ya kilimo viwandani.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inatekeleza malengo yake kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP) yenye lengo la kuleta mageuzi ya kilimo kutoka mtazamo wa uliopo wa kilimo cha kujikimu kufikia uendeshaji wa kilimo kwa mfumo wa kibniashara na hivyo kujzifanya shughuli za kilimo kuwa na manufaa kwa nchi na kuendana na dhamira ya kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.
Malengo mengine ya ASDP ni pamoja na kuongeza uzalishaji na tija ya kilimo hasa mazao ya biashara na mazao ghafi kwa uzalishaji viwandani ili kuchochea uwekezaji katika mnyororo mzima wa thamani wa uzalishaji wa mazao hayo kuendeshwa kibiashara na kusaidia kuongeza uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa na athari kwenye kilimo nchini.
Katika kuitikia wito wa Serikali wa kuendeleza mazao ya kimkakati ikiwemo zao la Korosho nchini, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania Naliendele Mtwara (TARI) imeanza utekelezaji wa maagizo hayo kwa kuanza kufanya tafiti mbalimbali zinazobainisha matumizi na thamani ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa kupitia korosho.
Akizungumza na Timu ya Maafisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO) waliofanya ziara kituoni hapo hivi karibuni, Kaimu Mkuu wa Kituo hicho Dkt. Fortunus Kapinga anasema kituo hicho kimejipanga kufanya utafiti unaolenga kutatua changamoto zenye kusaidia wadau kupitia mnyororo wa thamani unalenga katika uzalishaji na ubora wa mazao.
Dkt. Kapinga anasema kwa sasa Kituo hicho kinafanya utafiti wa kiekolojia inayohusisha hali ya udongo, hewa pamoja na mvua kuhusu maeneo husika yanayofaa kwa ajili ya kilimo cha zao la korosho, ambapo tayari Serikali imeanza elimu na teknolojia kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.
‘’TARI Naliendele tunajivunia kuongeza idadi ya Mikoa inayozalisha korosho kutoka Mikoa 5 hadi kufikia 17, ambayo ni Morogoro, Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Shinyanga, Katavi, Rukwa, Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga na Ruvuma ambapo tunaendelea kuwaelimisha wakulima kuhusu mahitaji halisi kuanzia kupanda hadi kula pamoja na matumizi ya zao hilo.’’ anasema Dkt. Kapinga.
Kwa mujibu wa Dkt. Kapinga Kituo hicho pia kinaendesha utafiti kuhusu matumizi ya tunda la bibo linalotokana na korosho ambalo wakulima wengi wamekuwa wakiyatupa kwani yamekuwa na matumizi mengine muhimu ikiwemo kutengeneza vinywaji mbalimbali ikiwemo juisi, wine na ethanol ambazo mahitaji ni makubwa katika masoko ya ndani nan je ya nchi.
Akifafanua zaidi Dkt. Kapinga anasema katika kilo moja ya korosho, tunapata kilo 9 za mabibo, ambayo yanazalisha lita 9 za juisi ya bibo, ambayo kitumia lita 9 za juisi ya bibo unaweza kutengeneza wine ya lita 4-5 ambayo kwa thamani inaweza kufika hadi Tsh 100,000, hivyo Kituo cha Utafiti cha Naliendele kimefanya utafiti huu na kinachotafuta kwa sasa ni kuweza kurasimisha utengenezaji wa wine ya mabibo uwe wa kibiashara na sio kutengeneza pombe ya kienyeji kama inavyotumika sasa.
Anaongeza kuwa hadi sasa Kituo hicho kimefanikiwa kuzalisha na mbegu mpya 54 za korosho zenye sifa ya kuzalisha kwa tija na kuvumilia magonjwa na wadudu waharibifu ambazo mkulima huweza kuvuna korosho kwa kipindi cha miezi minane baada ya kupanda shambani, hatua inayoifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika na duniani kuweza kusajili mbegu bora za korosho.
‘’Mbegu hizo tayari zimesambazwa katika mikoa na halmashauri zote nchini, ambapo mpango tulionao ni kusambaza miche Milioni 10 kila mwaka na kuhimiza halmashauri hizo kuzalisha miche Milioni 10 na kwa kufanikisha hili tunashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Bodi ya Korosoho ili kuhakikisha tunakidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi’’ alisema Dkt. Kapinga.
Akitoa tathimini ya mafanikio Dkt. Kapinga anasema katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 hadi 2020, kituo hicho kimeendelea kupata mafanikio makubwa kwa kuwa kumekuwa na mwitikio na ushiriki mkubwa wa kulima, kubangua, kusindika na kushiriki katika shughuli za kilimo cha zao la korosho kutokana na wananchi kutambua manufaa yake kiuchumi.
Anasema kuwa mafanikio hayo yametokana na mkazo uliowekwa na Serikali katika kutoa ajira kwa wataalamu wa kilimo na kutoa fedha za ufadhili wa utafiti wa mbegu bora, kwani tafiti nyingi za zao hilo zimekuwa zikihitaji muda na eneo kubwa katika kukamilika na kuleta matokeo yanayohitajika kitaalamu.
‘’Mtazamo wa Serikali kuhusu ardhi ulikuwa mzuri sana, hakuna nchi unayoweza kupewa ardhi zaidi ya ekari 900 lakini sisi TARI Naliendele tuna zaidi ya ekari 2000 katika maeneo ya Bagamoyo, Mkuranga, Nyangao, Namtumbo, Tunduru, Mbinga, Mnayoni yote haya ni mashamba yetu, ambapo katika mahesabu ya kawaida jaribio moja linahitaji ekari 25 na litafanyika kwa miaka 10-15’’ anasema Dkt. Kapinga.
Mkakati wa Serikali ni kutumia bidhaa zinazotengenezwa na viwanda vyetu vya ndani badala ya kutegemea bidhaa kutoka nje ya nchi, hivyo ili kufanikisha malengo hayo Taasisi za Umma na binafsi hazina budi kuunga mkono juhudi hizo kwa kuhakikisha kuwa kunawepo na mahusiano ya moja kwa moja na Sekta ya Viwanda kwa kuwa Viwanda ni soko la malighafi zinazozalishwa na Sekta ya kilimo.