******************************
Na Ahmed Mahmoud,Arumeru
Mwanamke mwenye familia ya watoto watatu, Rachel Kombe (48)Mkazi wa Kijiji cha Kiwawa,Embaseni wilaya ya Arumeru hana mahala pa kuishi baada ya kuondolewa kwenye nyumba na shemeji yake baada ya mume wake
kupatwa na matatizo ya akili.
Akizungumzia kadhia hiyo huku akibubujikwa na machozi ,amemwomba Rais John Magufuli kumsaidia aweze kurejea katika makazi yake kwani kwa sasa anaishi kwa kubangaiza yeye na watoto wake ambao ni wanafunzi.
Rachel alidai kwamba alianza kuishi katika eneo hilo yeye na mume wake ,Efhata Pallangyo(50) mwaka 1990 wakiwa na nyumba moja na baadaye waliongeza nyumba zingine za wapangaji.
Alisema mwaka 2014 shemeji yake aitwaye Elisaria Pallanyo alikuja nyumbani na kumchukua Mume wake akidai kwamba anaenda kumtafutia kazi maeneo ya umasini.
Hata hivyo mwaka 2015 Mme wake alipatwa na matatizo ya akili akawa hajitambui ndipo ndugu wa mumewe waliamua kumrejesha nyumbani kwa wazazi wake eneo la Pori wilayani humo anakoishi hadi sasa.
“Baada ya Mme wangu kupatwa na matatizo ya akili na kuondoka nyumbani ndipo shemeji yangu alianza kunifanyia vurugu ikiwemo kuchukua pikipiki mbili za mume wangu na kuziuza akidai mimi ni mchaga
hawanitaki na baadaye alinifungulia kesi mbalimbali akidai Mimi nimevamia nyumba ya mama yake, akitaka niondoke ” alisema Rachel.
Alisema kuwa katika kesi hizo ikiwemo ya baraza la Ardhi la kata na wilaya hakuwahi kushirikishwa ama kuitwa mahakamani ila ameshangaa juni 9 mwaka huu akiondolewa kimabavu katika nyumba yake huku vitu
vyake vikitupwa nje.
“Kwa sasa sina mahala pa kuishi mimi na wanangu wa kike akiwemo aliyefaulu kwenda kidato cha tano nashindwa nifanyeje nilienda kuomba nakala ya hukumu nikaambiwa nitoe lakimbili namimi sina hela namwomba
Rais Magufuli anisaidie jamani” amesema
Akiongelea tuhuma hizo Elisaria Pallangyo alidai kwamba mama huyo (Rachel)alivamia eneo hilo na kuanzisha makazi kinyume cha utatatibu kwani eneo hilo ni Mali ya mama yake mzazi aitwaye Yohane Pallangyo ambaye aligawiwa mwaka 1919 na chama cha ushirika cha Pori.
Hata hivyo alikanusha kwamba Ephata Pallangyo ambaye ni kaka yake kupatwa na matatizo ya akili akidai yupo nyumbani mzima na kwamba hafahamu kama Rachel alikuwa mke wa kaka yake.
“Kaka yangu hana matatizo ya akili yupo nyumbani mzima na sifahamu kama alikuwa na mke na watoto na kama watoto ni wa kaka kwanini huyo Mama asiwalete nyumbani”??, alihoji