Home Mchanganyiko KAMPUNI YA GODMWANGA YACHANGIA MIFUKO 70 YA SARUJI MIRADI YA AFYA,ELIMU

KAMPUNI YA GODMWANGA YACHANGIA MIFUKO 70 YA SARUJI MIRADI YA AFYA,ELIMU

0

*******************************

Kampuni ya Godmwanga inayochimba makaa ya mawe katika Kijiji cha Malini Kata ya Mtipwili Wilayani Nyasa, imetoa saruji mifuko 70,yenye thamani ya tsh milioni moja (1,000,000/=) kwa ajili ya kuchangia miradi mitatu ya afya na  elimu Kijijini hapo.

Saruji hiyo imekabidhiwa jana, katika viwanja vya ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Malini, na mwakilishi wa Mkurugenzi wa  kampuni ya Godmwanga, Bwana Alen Kimaro na kupokelewa na Wananchi wa kijiji hicho huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela Chilumba.

Akikabidhi Saruji hiyo, katika Mkutano wa Hadhara, bw kimaro alisema kuwa, kampuni inayochimba makaa ya mawe katika kijiji hicho kimethamini shughuli mbalimbali za maendeleo, zinazofanywa na wananchi pamoja na Serikali katika Kijiji hicho na Kampuni imejiridhisha , na kuwataka wananchi kuhakikisha saruji hiyo inatumika kama ilivyokusudiwa .

Aliongeza kuwa, saruji  ameitoa kwa mchanganuo, mifuko (50) ni kwa ajili ya Ukarabati wa Darasa la awali la shule ya Msingi Malini, Mifuko kumi ni kwa ajili ya Ukarabati wa Zahanati ya Chiulu na mifuko 10 kwa ajili ya Shule ya Msingi Mtipwili.

“Ndugu zangu Kampuni ya Godmwanga leo imeona itatue changamoto ya mifuko 70 ya saruji kama mlivyoomba, kwa kuwa sisi tunafanya kazi katika maeneo yenu kama mlivyotukaribisha  na ni wamoja na tunathamini shughuli za kimaendeleo mnazofanya, hasa za Utekelezaji wa Miradi ya maendeleo ya elimu na afya leo tumeona tuanze na mifuko 70 ya saruji na tutaendelea kuwaunga mkono kadiri mtakavoona inafaa” alisema kimaro

Alitoa wito kwa wananchi na makampuni mengine kuiunga mkono Serikali ya awamu ya Tano kwa kuchangia Miradi ya maendeleo ili kuboresha Huduma kwa wananchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela Chilumba aliipongeza kampuni hiyo, kwa kuchangia kiasi hicho cha saruji kwa kuwa msaada huo umetatua kero ya wananchi wa Kijij cha Malini na kuwaomba, waongeze juhudi za kushirikiana na Serikali pamoja na wawekezaji ili kujiletea maendeleo.Aidha alichangia tsh (300,000)ili kuunga mkono juhudi za maendeleo kijijini hapo.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Yohana Ndunguru kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho aliishukuru kampuni ya Godmwanga, kwa kutatua changamoto hiyo ya saruji  na kusema ni kweli walikuwa wanauhitaji wa saruji hiyo na atahakikisha inatumika vizuri.

Kampuni ya Godmwanga inachimba makaa ya mawe katika Kijiji cha Malini Kata ya Mtipwili Wilayani hapa  na kuuza sehemu mbalimba za nchi kama vile Kiwanda cha Dangote,Mbeya Cement na sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.