………………………………………………………………………………….
Na. Alex Sonna, Dodoma
MBUNGE wa Nanyamba(CCM), Abdallah Chikota ameitaka serikali kutatua changamoto ya uchakavu wa mitambo kwenye Skimu ya maji ya Makonde ili kuweza kusambaza maji kwa wananchi wa Mji wa Nanyamba.
Akiuliza swali bungeni , Chikota amesema kuwa Skimu hiyo inakabiliwa na tatizo kubwa la uchakavu wa mitambo na umeme usio wa uhakika na hivyo kushindwa kusambaza maji hadi Mji wa Nanyamba.
Katika majibu ya Wizara ya Maji, ameeleza kuwa eneo la Mamlaka ya Maji Makonde ina jumla ya watu 510,975 wenye mahitaji ya maji mita za ujazo 766,462 kwa mwezi.
Aidha Waziri huyo amesema kuwa maeneo yaliyofikiwa na miundombinu ya maji yana wakazi wapatao 275,928.00 wenye mahitaji ya maji mita za ujazo 413,892 kwa mwezi sawa na asilimia 54 ya mahitaji ya wakazi wote wa Mamlaka ya Maji Makonde.
“Miundombinu iliyopo inaweza kuzalisha maji mita za ujazo 482,400 kwa mwezi ambacho kinakidhi mahitaji ya watu wote waliofikiwa na mtandao wa maji,”amebainisha Waziri.
Pia ameongezea kuwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji na matengenezo, uwekezaji umepangwa kuelekezwa kwenye chanzo cha Mitema kwa kuwa chanzo hicho kina gharama za umeme nafuu zaidi katika uzalishaji maji.
“Uwezo wa chanzo hiki ni mkubwa kuliko vyanzo vingine na unaotosheleza mahitaji ya wakazi wote na kijiografia iko katikati ya eneo la Mamlaka ya Maji Makonde,”ameweka wazi .
Katika hatua nyingine Waziri amesema kuwa katika kuhakikisha wananchi wanaoishi maeneo yanayohudumiwa na Mamlaka ya Maji Makonde wanapata huduma ya maji, Serikali kupitia Wizara ya Maji ikishirikiana na Wadau wa Maendeleo imetoa kipaumbele katika uboreshaji wa huduma ya maji katika Mamlaka hiyo.
Hata hivyo, ilisema serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni jitihada za kukabiliana na tatizo la uchakavu wa mitambo.