Home Mchanganyiko HAKUNA MUDA WA NYONGEZA KWA WAKANDARASI WANAOTEKELEZA MIRADI YA REA

HAKUNA MUDA WA NYONGEZA KWA WAKANDARASI WANAOTEKELEZA MIRADI YA REA

0

Matukio katika picha zikimuonyesha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga wakati akikagua kazi za Mkandarasi wa Mtwara katika kijiji cha Mlingula kilichopo wilaya ya Masasi

………………………………………………………………………………..

Na. Alex Sonna,Dodoma

Wakandarasi wanaotekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza ambao mikataba yao itafikia ukomo Juni 30, mwaka huu wametahadharishwa kukamilisha miradi hiyo ndani ya muda uliopangwa kwa mijibu wa mikataba yao

Tahadhari hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, Mhandisi Amos Maganga katika kikao kazi cha kutathimini utekelezaji wa mradi huo katika mikoa ya Lindi na Mtwara kilichofanyika wilayani Ruangwa Juni 14 2020

Mhandisi Maganga amesisitiza kuwa hakutakuwa na nyongeza ya muda na itahesabika kuwa wameshindwa kazi hivyo zitapewa kampuni nyingine zimalizie kazi hizo.

Aidha Mhandisi Maganga metoa tahadhari hiyo baada ya Mkandarasi wa Mkoa wa Mtwara ambaye anajumuisha muungano wa kampuni za Radi Service LTD, Njarita Contractor LTD na Aguira Contractor Ltd kuomba kuongezewa muda wa miezi miwili hadi Agost 31, 2020 kwa ajili ya kukamilisha kazi iliyobaki.

“Muda wa mkataba uko palepale vinginevyo tutatafuta mtu mwingine atekeleze huo mradi..ndani ya siku 14 kazi iwe imekamilika mkishindwa tutawanyang’anya kazi,” ameweka wazi Mhandisi Maganga.

Mhandisi Maganga ameagiza wakandarasi wote kuongeza magenge ya kazi ili waweze kukamilisha kazi ndani ya siku 14 zilizobaki na wakabidhi mradi huo.

Akiomba kuongezewa muda, Mkandarasi ws Mtwara, Mhandisi Ahmed Hemed amesema kuwa walipata changamoto ya vifaa kutoka nje ya nchi hivyo kupelekea kukwama kukamilisha mradi kwa wakati hivyo na kuomba kuongezewa muda wa kukamilisha mradi huo.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Maganga amempongeza Mkandrasi wa Mkoa wa Lindi kampuni ya State Grid kwa hatua nzuri ya kutekeleza mradi kwa asilimia 92 ambapo ameshaunganisha umeme katika vijiji 113 kati ya vijiji 133 vya mkataba wake na kuwa vijiji 20 vilivyobaki vipo katika hatua za mwisho za kuunganishiwa umeme.

Awali Mhandisi Maganga alikagua mradi wa kuweka taa za barabarani unaofadhiliwa na Wakala waNishati Vijijini (REA) na kuagiza mradi huo uwe umekamilika ifikapo Julai 16 ,2020 na kuwa hawataongeza muda tena.

Mhandasi Maganga amesema kuwa  lengo la mradi huu ni kuibua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Ruangwa kwa kuwawezesha kufanya biashara kwa muda mrefu zaidi n kuboresha usalama wa mji huo.