Vyama 12 DP,NRA, AAFP, UMD, UDDP, Makini, TLP,UDP, SAU, NLD, ADC, na CCK, visivyokuwa na wawakilishi bungeni, vimetangaza kushirikiana katika uchaguzi mkuu, kwenye ngazi ya ubunge na udiwani, kwa kufanya kampeni pamoja na vimeamua kusimamisha wagombea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa umoja huo, Rashid Rai alisema: “Tunatangaza kushirikiana katika uchaguzi mkuu kwenye ngazi ya udiwani na ubunge, tutasimamisha mgombea kwenye kila jimbo”.
Kuhusu nafasi ya mgombe urais, Rai alisema kila chama kitafanya mkutano mkuu na kuamua namna ya ushirikiano na kwamba vitatoa matakamko kuhusu nafasi hiyo.
“Tumemsikia Katibu Mwenezi na Itikadi wa Chama Cha Mapinduzi, Humprey Polepole, akizungumzia masuala ya rushwa katika chama chake, tunamuomba suala la rushwa lisiishie katika uteuzi tu, bali waendelee hadi kwenye ngazi ya uchaguzi,” alisema Rain a kuongeza:
“Tunataka suala la kupinga rushwa liende hadi kwenye sanduku la kupiga kura, suala la kupita bila kupingwa nalo tutalihesabu kama sehemu ya rushwa kwa sababu haiwezekani mgombea apite bila ya kupingwa,” alisema Rai.
Aidha, aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuhakikisha inakuwa macho katika kuwakamata na kudhibiti vitendo vya baadhi ya wagombea ambao wamejiandaa kutoa rushwa kwa wananchi.
Alisema rushwa ni mojawapo ya jambo linaloharibu uchaguzi mkuu na kwamba wagombea wasiokuwa na sifa ndiyo wanaochaguliwa kwa kutoa rushwa.
Mwenyekiti wa umoja huo, Hassan Almas, alisema kwenye kila jimbo vyama vyao vitashirikiana kwa kupiga kampeni kwa pamoja na kwamba kila mgombea atakapokuwa anafanya kampeni atakuwa na bendera za vyama vyote.
Alisema kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, umoja huo umeamua kusimamisha mgombea kwenye kila jimbo na kwamba watahakikisha mgombea atakayeteuliwa kukiwakilisha chama amechaguliwa na wajumbe wa vyama vyao.
Naye Katibu wa umoja huo, Abdul Mluya, akizungumzia kuhusu tukio la vyama vya siasa kusaini maadili ya uchaguzi alisema: “Tulisaini pasipo kulazimishwa, sisi tulisaini baada ya kuona maadili yapo vizuri, sasa hao wanaolalamika kwamba walilazimishwa tunawashangaa”.
Alisema wakati wa kusaini maadili hayo hakuna chama kilicholazimishwa na kwamba baadhi ya vyama wanataka kufanya mchakato wa uchaguzi kuwa ni suala la kwao peke yao jambo ambalo siyo kweli kwani ni suala linalowashirikisha wananchi.
Aidha, aliwataka Watanzania kuwa makini na wagombea watakaowafuata wakati wa kampeni na kuwaomba kura kwa sababu wengi wao watakuja na hoja za udanganyifu.