…………………………………………………………………..
Dar es Salaam,
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa hali ya hewa wa msimu wa kipupwe hapa nchini, unaoanzia Mwezi Juni – Agosti 2020, taarifa hiyo imeelezea athari zinazoweza kujitokeza pamoja na ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumzia msimu huo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliwataka wananchi kufuatilia utabiri huo wa msimu wa kipupwe kwa kipindi cha Juni-Agosti (JJA) 2020, ambapo mvua za msimu wa Machi hadi Mei ambazo zilileta athari hapa nchini zimeisha.
“Msimu huu wa kipupwe unatarajiwa kuwa na vipindi vifupi vya upepo mkali wa Kusi na hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchi, hata hivyo, vipindi vya baridi kali vinatarajiwa katika maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kusini-magharibi hususan nyakati za usiku na asubuhi”. Alisema Dkt. Kijazi
“Vipindi vya baridi kali vinatarajiwa hasa katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Juni na kupungua kuelekea mwishoni mwa msimu yaani mwezi Agosti kwa maeneo ya mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Rukwa pamoja na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Ruvuma, maeneo haya yanatarajiwa yatakuwa na joto la kawaida kati ya nyuzi joto 6 na 12, hata hivyo baadhi ya maeneo hususan katika mikoa ya Njombe na Mbeya yanatarajiwa kuwa na joto la chini ya nyuzi joto 6”. Aliongezea Dkt. Kijazi
“Nawakumbusha wananchi kuchukua tahadhari na kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama unavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania”, alisisitiza Dkt. Kijazi
Akitoa ufafanuzi zaidi, Dkt. Kijazi alielezea hali ya joto katika maeneo mengi hapa nchini, huku akibainisha kuwa joto la kawaida linatarajiwa katika maeneo mengi ya ukanda wa Pwani na kuashiria uwepo wa vipindi vichache vya baridi ikilinganishwa na hali ya wastani wa muda mrefu (1981-2010) kwa miezi ya Juni-Agosti katika maeneo hayo.
Akizungumzia kuhusu mvua, Dkt. Kijazi alisema, vipindi vya Upepo unaovuma kutoka mashariki na kusini mashariki (Matlai) vinatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika bahari ya Hindi na kusababisha kuwepo na matarajio ya vipindi vifupi vya mvua nyepesi katika maeneo machache.
Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Kijazi alisema, hali ya ukavu na upepo inaweza kuongeza upotevu wa maji kwa njia ya mvukizo na kuathiri upatikanaji wa maji kwa mazao, mifugo na matumizi mengine. Jamii inashauriwa kuzingatia matumizi endelevu ya maji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
“Jamii inashauriwa kuzingatia matumizi endelevu ya maji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza, wakati huohuo wakizingatia tahadhari za upepo mkali ambazo zitaendelea kutolewa na TMA kila upepo mkali utakapojitokeza”. Alimalizia Dkt. Kijazi