Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Nane ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi uliofanyika katika ofisi za VETA Makao Makuu, jijini Dar es Salaam .
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akipokea nakala ya kitabu cha kufundishia mfumo wa sayari kwa shule za msingi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu. Kitabu hicho kimeandikwa na mbunifu wa mfumo wa kufundishia sayari wa Chuo cha VETA Dar es Salaam Bw. Ernest Maranya.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, akimkabidhi vitendea kazi, Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Bw. Peter Maduki, wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika katika ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Nane ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Menejimenti ya VETA mara baada ya kuzindua Bodi ya Nane ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Nane ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi mara baada ya kuzindua Bodi hiyo katika hafla iliyofanyika kwenye ofisi za VETA Makao Makuu jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akipata maelezo kuhusiana na bidhaa za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa COVID 19 zinazozalishwa na Chuo cha VETA Dar es Salaam, alipowasili kwenye uzinduzi wa Bodi ya Nane ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi
*************************
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Prof. Joyce Ndalichako, ameiagiza Bodi mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi yanawafikia Watanzania wengi zaidi ili kutatua changamoto ya ajira kwa vijana na kuchochea kasi ya uanzishwaji wa viwanda nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Nane ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, tarehe 8 Juni, 2020, Prof. Ndalichako amesema kuwa elimu na mafunzo ya ufundi stadi ni moja ya maeneo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele na kutiliwa mkazo zaidi katika kujenga uchumi wa viwanda ili kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa Viwanda.
Prof. Ndalichako ameiagiza Bodi hiyo kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi mbalimbali inayosimamiwa na VETA, hasa ujenzi wa vyuo vya VETA vya Wilaya 29 unaoendelea hivi sasa na uboreshaji wa vyuo vilivyopo kwa kukarabati na kujenga madarasa, karakana na mabweni zaidi ili kutoa fursa kwa Watanzania wengi hasa vijijini kupata mafunzo hayo muhimu.
“Tunataka mafunzo haya ambayo yameonekana ni mkombozi kwa wananchi, hasa vijana, yawafikie Watanzania wengi zaidi. Hivyo Bodi hii ina kazi kubwa ya kusimamia ukamilishwaji wa ujenzi wa vyuo vya VETA unaoendelea katika Wilaya mbalimbali nchini”, alisema.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, amesema kuwa Bodi iliyomaliza muda wake mwezi Februari, 2020 ilikuwa na mafanikio mengi kwa kipindi chake cha miaka mitatu (2017 -2020), ikiwemo ongezeko la vyuo vinavyotoa mafunzo ya Ufundi Stadi nchini kutoka 451 hadi 684 na vyuo vinavyomilikiwa na VETA kutoka 29 hadi 41, kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi wa ufundi stadi kutoka 169,118 hadi 302,369 na kusimamia shughuli mbalimbali za ubunifu hadi kuzalisha bidhaa halisia ambazo baadhi yake zimeingia sokoni.
Dkt Bujulu ametoa mfano wa mbunifu Ernest Maranya wa Chuo cha VETA Dar es Salaam ambaye amebuni kifaa cha kufundishia mfumo wa sayari na kutunga kitabu cha kufundishia mfumo huo kwa shule za msingi. Mkurugenzi Mkuu amemkabidhi Mhe. Waziri nakala ya kitabu hicho.
Hata hivyo, Dkt. Bujulu ameainisha changamoto kadhaa na kumuomba Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia awasaidie kuzitatua. Miongoni mwa changamoto hizo ni uchakavu wa miundombinu ya vyuo vikongwe vya VETA; kutotosheleza kwa miundombinu ya sasa, hasa mabweni; gharama kubwa za kuiwezesha VETA kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia duniani na fedha za kujenga vyuo vya VETA katika maeneo mengi zaidi ili kukidhi kiu ya Watanzania walio wengi wanaohitaji mafunzo ya ufundi stadi kwa ajili ya kujikwamua kimaisha na kutoa mchango katika maendeleo ya viwanda nchini.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Peter Maduki, aliyeteuliwa kwa mara ya pili kuongoza Bodi hiyo, ameahidi kuwa Bodi yake itatekeleza majukumu waliyopewa kwa bidii na weledi mkubwa na kufanyia kazi maelekezo ya Mheshimiwa Waziri ili kuboresha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Bodi ya nane ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi itahudumu kwa muda wa miaka mitatu (2020 – 2023) na wajumbe wake ni Bw. Peter Maduki (Mwenyekiti), Bw.Ally A. Msaki (Mkurugenzi wa Ajira, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu); Dkt. Ethel Kasembe (Naibu Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia); Dkt. Michael Mawondo (Mwenyekiti wa RAAWU Taifa); Padre Dkt. Francis Xavier Ng’atigwa (Mjumbe kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania) na Bi. Clotilda Timothy Ndezi (Mkurugenzi wa Programu za Maendeleo na Uhamasishaji, Jumuiya Ya Kikristo Tanzania, CCT).
Wengine ni Bw. Nuhu Mruma (Katibu mkuu, BAKWATA); Bi. Anna Kimaro (Mtaalamu wa Sera za Mazingira ya Biashara, Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania, CTI); Bw. Paul Faraj Koyi (Rais wa Chama cha wenye Viwanda, Biashara na Kilimo Tanzania, TCCIA); Bi. Leah Ulaya (Rais wa Chama cha Walimu Tanzania, CWT) na Dkt. Pancras Bujulu (Mkurugenzi Mkuu wa VETA, ambaye ni Katibu wa Bodi).