Home Mchanganyiko VIFO TAKRIBANI 125,000 HUTOKEA KILA MWAKA KWA WATOTO WENYE UMRI WA MIAKA...

VIFO TAKRIBANI 125,000 HUTOKEA KILA MWAKA KWA WATOTO WENYE UMRI WA MIAKA 5 KWA MAGONJWA YATOKANAYO NA KULA CHAKULA KISICHO SALAMA-BW.MSASALAGA

0

Mkurugenzi wa udhibiti Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania TBS, Bw.Lazaro Msasalaga akizungumza na Wanahabari katika Ofisi za shirika hilo Jijini Dar es Salaam leo.

*************************************

NA EMMANUEL MBATILO

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) juu ya makadirio ya tatizo la magonjwa yatokanayo na chakula kisicho salama zilitolewa mwaka 2015 zinaonesha kuwa mtu 1 kati ya 10 duniani huugua kila mwaka kutokana na kula chakula kisicho salama na husababisha vifo vya watu takribani 420,000

Ameyasema hayo leo Mkurugenzi wa udhibiti Ubora TBS, Bw.Lazaro Msasalaga katika kikao cha waandishi wa habari kilichofanyika katika ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam.

“Magonjwa haya yameripotiwa kuathiri zaidi watoto walio chini ya umri wa miaka 5,ambapo inakadiriwa kusababisha vifo takribani 125,000 kila mwaka”. Amesema Bw.Msasalaga.

Pamoja na hayo Bw.Msasalaga amesema takwimu hizo zinaonesha kuwa tatizo hilo ni kubwa zaidi katika bara la Afrika, ambapo inakadiriwa watu zaidi Milioni 9 huugua na 137,000 kufa kila mwaka.

Aidha, amesema kuwa kwa hapa nchini madhara mbalimbali yanayohusishwa na ulaji wa chakula kisicho salama yamekuwa yakiripotiwa katika matukio mbalimbali.

“Magonjwa yatokanayo na chakula kisicho salama yanaweza kuzuilika iwapo kila mmoja wetu atatekeleza wajibu wake katika mnyororo wa chakula”. Amesema Bw.Msasalaga.

Bw.Msaalaga amesema kwa kutambua umuhimu wa chakula salama,TBS imeweka mifumo ya kiudhibiti ili kuhakikisha chakula kilichopo katika soko hapa nchini ni salama ili kulinda jamii dhidi ya madhara yatokanayo na kula chakula kisicho salama.

.