Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza mjini Babati
…………………………………………………………………………………..
Sakata la Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara, Ester Mahawe kupewa adhabu ya uangalizi kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kudaiwa kuanza kampeni kabla ya muda kwenye Jimbo la Babati Mjini limechukua sura mpya baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kuingilia kati.
Mkuu wa TAKUKURU wa mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu alisema kwa mujibu wa kanuni za CCM za viongozi waliopo madarakani, mbunge huyo Mahawe hakufanya kosa linalostahili adhabu hiyo.
Makungu alisema kwa mujibu wa kanuni hiyo ya chama tawala wabunge ambao wapo madarakani wana haki ya kuhudumia jamii wanayoiongoza hadi Bunge litakapovunjwa hivyo Mahawe hana kosa.
Alisema kanuni hiyo inasema ni marufuku kwa mwanachama yeyote anayetarajia kugombea au wakala wake kutoa misaada mbalimbali wakati uchaguzi unapokaribia ambayo dhahiri ina lengo la kuvutia kura isipokuwa Rais, mbunge, mwakilishi au diwani.
Alisema kanuni hiyo ya 69 kifungu cha sita cha uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola kupitia CCM kinatoa mamlaka kwa viongozi hao waliopo madarakani kwa kuwa bado wana wajibu wa kuhudumia maeneo yao ya uongozi.
“Endapo itampendeza mbunge Mahawe na akiwa mjini Babati alete malalamiko yake rasmi TAKUKURU ili tuyachunguze kwa kuzingatia kanuni za chama chake juu ya wabunge waliopo madarakani,” alisema Makungu.
Mara baada ya habari za mbunge huyo Mahawe kuandikwa, watu mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii hasa ya wanachama wa CCM wa mjini Babati ilizizima kwa kujadili habari hizo.
Mfanyabiashara maarufu wa kuuza biriani wa mjini Babati, Zulekha Mohamed alihoji kwenye mitandao hiyo kuwa Mahawe ni mbunge wa viti maalum kwa nini anagawa misaada kwa wapiga kura na siyo kaya maskini au watoto yatima hiyo siyo kampeni?
Mjumbe wa baraza la jumuiya ya wazazi wa CCM Taifa kupitia mkoa wa Manyara, Wilbroad Bayo akizungumza kwenye mitandao hiyo alisema Mahawe ni mbunge kwa mujibu wa katiba ana haki ya kutembelea wilaya tano za mkoa huo.
Bayo alisema hakuna haki inayomnyima Mahawe kutoa huduma za kijamii ndani ya wilaya ya Babati mjini kwa kofia yake ya mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Manyara kupitia CCM.
“Wapo wanaotembelea magari ya rushwa tunawaangalia tuu lakini kutoka katika sakafu ya moyo wangu muda utaongea na mbunge wa jimbo la Babati mjini atapatikana,” alisema.
Diwani wa viti maalum wa Tarafa ya Dongobesh wilayani Mbulu Ester Joel alisema kamati ya maadili ya CCM wilaya ya mjini Babati haina mamlaka ya kutoa adhabu hiyo kwa Mahawe kwani ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM ya mkoa huo.
Hivi karibuni kamati ya maadili ya CCM ya wilaya ya Babati mjini ilimpa Mahawe adhabu ya uangalizi kwa kipindi cha miezi 12 kwa kudaiwa kuanza kampeni kabla ya muda na kutoa rushwa na viongozi wengine saba kupewa onyo kwa kuanza kampeni ya ubunge na udiwani katika eneo hilo kabla ya muda.