Na.Mwandishi wetu,Dar es Salaam
MWENYEKTI wa Yanga SC, Dk. Mshindo Msolla amezindua Kampeni ya kuelekea kwenye mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Klabu.
“Moja ya ajenda zangu wakati nagombea uongozi ilikuwa ni kuhakikisha tunaingia kwenye mabadiliko ya mfumo mpya wa uendeshaji wa Klabu yetu.
“Leo nina furaha kuzindua kampeni hii ambayo ni hatua muhimu kuelekea kwenye matukio makubwa ya mabadiliko tunayoyatarajia,” amesema.
Amesema kampeni hiyo yenye Kaulimbiu ‘Twenzetu kwenye Mabadiliko’ inashirikisha Wanayanga wa kada mbalimbali na itakuwa ikirushwa na Azam TV pamoja na Channeli za Yanga.
“Lengo la kampeni hii ni kuwaandaa Wanayanga juu ya ujio wa matukio makubwa kuelekea kwenye mabadiliko ya mfumo wa Klabu yetu,” amesema.
Dk. Msolla amesema mchakato wote wa mabadiliko unafanyika kwa udhamini wa Kampuni ya GSM ambayo imejitolea kuisaidia Yanga katika suala hilo.
“Tunawashukuru sana wadhamini wetu kampuni ya GSM ambao wameamua kudhamini na kuubeba mchakato huu, na kwa kukubali ombi la Kamati ya Utendaji kutusaidia kuingia kwenye mabadiliko.
“Wanayanga wote, Wanachama, Mashabiki na wapenzi wote tuungane kutimiza jambo hili muhimu kwa manufaa ya Klabu yetu,” amesema.
Kuzinduliwa kwa kampeni hii ni hatua muhimu kuelekea kwenye mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji kwa Klabu ya Yanga ambapo matukio kadhaa sasa yatafuata kabla ya Wananchi kufanya maamuzi ya Kikatiba kuridhia mfumo mpya.