Maafisa tarafa za Tarafa 12 za mkoa wa Ruk2wa wakiwa kila mmoja amesimama nyuma ya Pikipiki tayari kwa kukabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Afisa Tarafa wa Tarafa ya Namanyere Wilayani Nkasi Kasim Ibrahim akitia saini hati ya Makabidhiano mbele ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa ili kukabidhiwa Pikipiki aliyoahidiwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Katibu Tawala wa MKoa wa Rukwa Benard Makali akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo bahasha yenye funguo za Pikipiki ili aweze kutoa Pikipiki kwa Afisa Tarafa (hayupo pichani)kwa niaba ya maafisa tarafa wenzie.
Uongozi wa Mkoa wa Rukwa ukiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo wakiwa katika picha ya pamoja na Maafisa Tarafa wa mkoa baada ya makabidhiano ya Pikipiki zilizotolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
……………………………………………………………………..
Katika hatua za kuboresha utendaji kazi wa Maafisa Tarafa nchini Rais Wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John pombe Magufuli ametoa pikipiki 12 kwa Maafisa Tarafa mkoani Rukwa ili ziweze kuwasaidia kutekeleza majukumu yao ya kiserikali katika kata wanazozihudumia.
Pikipiki hizo zimetolewa ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa tarehe 04.06.2019 baada ya kufanya kikao kazi na Maafisa Tarafa wote nchini alipokutana nao Ikulu Jijini Dar es salaam.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi pikipiki hizo Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alimshukuru Rais kwa kutimiza ahadi hiyo huku akiwasisitiza maafisa hao kuzitumia pikipiki hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na Rais ikiwemo kusimamia mapato, miradi ya maendeleo iliyopo kwenye maeneo yao pamoja na kusikiliza kero za wananchi.
Alieleza kuwa katika ziara zake alizozifanya katika maeneo ya vijijini, alibaini kuwepo kwa mwamko mdogo wa wananchi juu ya ugonjwa hatari wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) hivyo kuwataka maafisa hao kuhakikisha wanavitumia vyombo hivyo kufikisha elimu ya ugonjwa huo hatari.
“Ni Imani yangu kuwa tutavitumia vyombo hivi vya usafiri kuhakikisha kuwa tunawafikia wananchi wetu kwenye maeneo yao ili tuweze kuwahamasisha kujikinga na ugonjwa huu hatari ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka mara kwa mara na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima,” Alisema
Aidha, Alimtaka Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa kuhakikisha anachukua hatua kali za kisheria na kiutumishi kwa Afisa Tarafa yeyote atakayetumia pikipiki hiyo kinyume na malengo ya serikali ikiwemo kutumia kama Bodaboda na kuongeza kuwa pikipiki hizo zina namba za serikali, hivyo, kuzitumia kinyume na malengo yake ni ukosefu wa maadili.
Kwa upande wake Katibu Tawala huyo wakati akieleza mgawanyo wa pikipiki hizo alisema kuwa Mkoa wa Rukwa una Tarafa 16 ambapo Tarafa 4 kati ya hizo zina pikipiki ambazo zimekaguliwa na ziko salama zinaendeelea kufanya kazi na hivyo kuwasisitiza maafisa hao kutekeleza majukumu yao kama yalivyoainishwa katika Waraka Namba 1 wa Maendeleo ya Utumishi wa Umma wa Mwaka 2007.
“Tarafa ambazo hazikuwa na usafiri kwa wilaya ya Kalambo ni Tarafa ya Matai, Kasanga, Mwimbi, Mwazye na Mambwenkoswe zilikuwa hazina usafiri. Kwa Wilaya ya Sumbawanga ni Tarafa ya Itwelele, Kipeta, Lwiche na Mtowisa na Wilaya ya Nkasi ni Tarafa ya Chala, Kate na Namanyere na tarafa ambazo zilikuwa na pikipiki kwa Wilaya ya nkasi ni Wampembe na Kirando na Wilaya ya Sumbawanga ni Laela na Mpui,” Alisema.
Wakati akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Maafisa Tarafa wenzake, Afisa Tarafa ya Kasanga Andrew Ngindo baada ya kumshukuru Rais Magufuli, alimuomba Mkuu wa Mkoa kuona uwezekano wa kutengewa bajeti ya mafuta pamoja na matengezo kwa pikipiki hizo ili ziendelee kuwarahisishia utekelezaji wa majukumu yao.
“Kuwa na Pikipiki ni jambo moja lakini pikipiki ikiwa bila ya Mafuta bila ya uwezeshwaji wa kutosha ni kama tembo mweupe ndani ya nyumba, mimi niwaombe sana wakuu wa wilaya, sisi ndio wawakilishi wao katika maeneo yale ambayo wao wasipofika sisi tukifika maana yake Mkuu wa Wilaya amefika na tayari tumekuwa tumetekeleza makujumu yao, kwahiyo Wakuu wa wilaya watusaidie kupata bajeti hiyo,” Alisema.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe magufuli aliahidi kuwapa usafiri maafisa tarafa wote nchini wasio na usafiri na hivyo kutoa pikipiki 448 kote nchini kwaajili ya maafisa hao ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake.