Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo akizungumza na wandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma leo wakati akitangaza ajira za madaktari wapya 610
…………………………………………………………………
Na.Alex Sonna, Dodoma
SERIKALI imeajiri Madaktari wapya 610 ili kwenda kuongeza kasi katika utoaji wa huduma za afya katika Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo wakati akitangaza ajira hizo.
Mhe.Jafo amesema kuwa waajiriwa wote waliopata nafasi hizo wanatakiwa kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi walivyopangiwa kuanzia Mei 11 hadi 25 Mwaka huu wakiwa na nyaraka zao zote muhimu.
Mhe.Jafo amewaagiza Wakurugenzi wote nchini ambao madaktari hao wamepangiwa kwenye halmashauri zao kuhakikisha wanawaandalia stahiki zao muhimu punde tu watakaporipoti bila kuwacheleweshewa.
Aidha Mhe. Jafo amewataka pia Wakurugenzi hao kutowabadilishia vituo vya kazi madaktari hao kwa kuwapeleka katika vituo wanavyovitaka wao kwani wamepangiwa kulingana na mahitaji ya maeneo husika.
” Niwatake Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuzingatia maelekezo haya, wasiwabadilishie madaktari hawa vituo ambavyo washapangiwa. Siyo Daktari amepangiwa Hospitali ya Wilaya Mkurugenzi anamhamishia kwenye Kituo cha Afya”, ameeleza Mhe.Jafo.
Mhe. Jafo ametoa wito kwa madaktari ambao wamepata ajira hizo kufanya kazi kwa weledi mkubwa wakijua kwamba wameaminiwa kuwahudumia wananchi.
“Siyo wanachukua posho na mshahara halafu wanaanza kuleta visingizio vya kuacha kazi,” amesisitiza Mhe. Jafo.
Katika hatua nyingine Mhe. Jafo amemshukuru Rais Magufuli kwa namna ambavyo ameiboresha sekta ya afya kwa kugawa ajira nyingi ndani ya muda mchache sambamba na kujenga vituo vingi vya Afya pamoja na Zahanati.
Ajira hizi 610 zimeifanya sasa orodha ya madaktari ambao wameajiriwa kwenye miaka minne ya Serikali ya Rais Magufuli kufikia 9839 na hii ni kwa Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati ambazo hizi zinasimamiwa na Wizara ya TAMISEMI.
ikumbukwe kuwa Tangazo la ajira za madaktari hao zilitolewa Machi mwaka huu ambayo mchakato wa kuwapata ulifanyika hadi Aprili mwaka huu kwa kuzingatia vigezo mbalimbali katika kupata madaktari mahiri.