Home Mchanganyiko UGONJWA WA CORONA BADO UPO TANZANIA, ENDELEENI KUCHUKUA TAHADHARI

UGONJWA WA CORONA BADO UPO TANZANIA, ENDELEENI KUCHUKUA TAHADHARI

0

Waziri Ummy Mwalimu akiongea na mwananchi kupitia kituo cha afya cha huduma kwa wateja mara baada ya kukizindua

Waziri Ummy Mwalimu akiongea wakati wa uzinduzi huo

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiangalia namna watoa huduma wanavyopokea simu kutoka kwa wananchi kwa ajili ya kupata elimu kuhusu ugonjwa wa Corona

Muonekano wa kituo cha afya cha huduma kwa wateja ambacho kitakua na wataalam 150 wa kutoa elimu na taarifa kwa wananchi

………………………………………………………………………….

Na. Catherine Sungura,WAMJW,Dar es Salaam.

Serikali itaendelea kutoa takwimu za mwenendo kuhusu Ugonjwa wa Corona mara baada ya kukamilika kwa maboresho ya kiufundi ya Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akizindua kituo cha Afya cha huduma kwa wateja (Afya call center) kilichopo eneo la Chuo cha Afya ya Sayansi ya Jamii Muhimbili (MUHAS), upanga Dar es Salaam.

“Takribani siku Saba sasa hatukuweza kutoa taarifa za takwimu za maabara  kuhusu mwenendo wa Corona nchini kwa sababu sasa hivi tunafanya maboresho  ya  maabara ya taifa ya afya ya jamii,hivyo niwatoe hofu wananchi kwamba ndani ya siku chache zoezi litakamilika na tutaendelea kutoa taarifa kwa umma mara kwa mara”, alisema.

Waziri Ummy amesema kuwa Corona ipo na itaendelea kuwepo kwa  miezi kadhaa,pia kumekuwepo na vifo kutokana na ugonjwa huu, hivyo wananchi wanapaswa kujua namna ya kuishi na ugonjwa huo kwa kujikinga na maambukizi.

 “Ninawasihi wananchi muondoe hofu na muendelee kuchukua tahadhari  ya kujikinga kwani ugonjwa wa Corona bado upo Tanzania, wagonjwa wapo na vifo vinavyotakana na COVID-19  vipo, ni muhimu kutambua kuwa ugonjwa huu utaendelea kuwepo kwa miezi kadhaa hivyo lazima mchukue tahadhari ya kujikinga kama magonjwa mengine”Alisisitiza Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amewataka wananchi kuendelea na  shughuli zao za ujenzi wa Taifa za kila siku pamoja na kuchukua tahadhari kwa  kuepuka  mikusanyiko isiyo ya lazima, kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka, na kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu mwingine.

Kuhusu Uvaaji wa barakoa, Waziri huyo amewataka wananchi kuendelea kuvaa   barakoa za vitambaa ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo na kuwa barakoa za viwandani ziachwe zitumike kwa ajili ya watoa huduma za afya.

Amewashauri wananchi kufua na kupiga pasi barakoa za vitambaa kabla ya kuzitumia na kusisitiza kuwa zinapaswa kuwa safi kabla ya kuvaliwa.

MWISHO