Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma ambapo ameomba kutengewa kiasi cha sh. bilioni 40.1 kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Mbunge wa Chemba Juma Nkamia akichagangia hoja wakati wa kujadili bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Wabunge wakiendelea na mjadala wa bajeti ya bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Watendaji wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakifuatilia mjadala wa hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 bungeni Jijini Dodoma.
(Picha na Eleuteri Mangi-WHUSM, Dodoma)
………………………………………………………………………………………….
Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Dodoma
Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 imeongezeka hadi kufikia kiasi cha sh. bilioni 40.1 kutoka sh. Bilioni 30.9 kwa mwaka wa fedha uliopita ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Akiwasilisha hotuba ya Bajeti hiyo Bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa ongezeko la sh. bilioni 9.2 ambalo ni sawa na zaidi ya asilimia 29.2 itaenda kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Katika mwaka wa fedha ujao fedha zitaenda kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika yenye kiasi cha sh. milioni 515, Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kilichotengewa sh. milioni 250 kwa ajili ya ukarabati wa chuo hicho pamoja na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kiasi cha sh. milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni pamoja na viwanja vya michezo”, alisema Mhe.Mwakyembe.
Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa miradi mingine itakayotekelezwa ni ujenzi wa eneo Changamani la michezo Dar es Salaam na Dodoma ambao umetengewa kiasi cha sh. milioni 650, mradi wa upanuzi wa usikivu redio za TBC Taifa na TBC FM ambao umetengewa kiasi cha sh. bilioni 5 pamoja na mradi wa Habari kwa Umma ambao umetengewa kiasi cha sh. bilioni 1 inayofanya miradi yote kutekelezwa kwa jumla ya sh. bilioni 7.7.
Akizungumzia sekta ya michezo, Mhe.Waziri amesema kuwa ni sekta ambayo inaimarisha afya na kulitangaza Taifa ndio maana leo nchi inasikika katika matangazo ya Premier League na UEFA kupitia vijana wanaocheza michezo ya kulipwa nje ya nchi akiwemo Mbwana Samatta pia mafanikio ya timu ya wanawake ya mpira wa miguu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.Hassan Abbasi amesema kuwa Serikali imefanya mambo makubwa kwa sekta za Wizara hiyo muhimu kwa nchi, na fedha zilizopitishwa zitaenda kuboresha mkakati wa kuitangaza lugha ya Kiswahili ambayo ni bidhaa adhimu Duniani kwa kuwekeza kununua vifaa vya ukalimani, kufundisha wakalimani, kutengeneza vitabu ambavyo vitakuwa ni miongozo ya ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wageni.
“Kwa mara ya kwanza tumepata bajeti kwa ajili ya taasisi yetu ambayo ni Kampuni yetu ya Magazeti ya Serikali (TSN) ambayo kwa miaka mingi ilikuwa inajitegemea na kujiendesha kibiashara lakini kwa sasa Serikali imefanya uamuzi TSN watalipwa mishahara na Serikali ili waweze kuwekeza katika maeneo mengine”, alisema Dkt. Abbasi.
Aidha, Dkt. Abbasi alifafanua kuwa mafanikio yaliyopo katika Wizara hiyo yametokana na ushirikiano ambao inaupata kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo vyombo vya habari na wanahabari, wasanii, wanautamaduni na wanamichezo wote nchini.
Akichangia mjadala wa bajeti hiyo, Mhe. Amina amesema kuwa usimamizi mzuri na utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo umefanya sekta zake zifanye vizuri ikiwemo sekta ya habari ambayo tofauti na nchi nyingi Duniani, Tanzania ina jumla ya televisheni zilizosajiliwa 44 pamoja na vituo vya redio 186.
Kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Wizara inatarajia kukusanya jumla ya shilingi 960,000,000 kupitia Idara ya Habari – MAELEZO na Maendeleo ya Michezo, kwa upande wa Taasisi saba zilizo chini ya Wizara, kiasi kinachokadiriwa kukusanywa ni jumla ya shilingi 40,171,264,000.