………………………………………………………………….
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
MKUU wa Mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evaristi Ndikilo amepokea msaada wa mifuko 40 ya sabuni kwa ajili ya kituo cha matibabu ya Wagojwa wa COVID 19 ambayo ni Hospitali ya Wilaya ya Kibaha Mjini.
Msaada huo umetolewa na kampuni ya KEDS Group Limited ,ikiwa ni jitihada za kuunga mkono juhudi za serikali kuendelea kupambana na ugonjwa wa corona .
Akipokea Msaada huo ,Mhandisi Ndikilo aliishukuru Kampuni ya KEDS Group Limited na kusema kwani sabuni hizo zitatumika kusafishia majengo na kufulia nguo za madaktari.
Aidha aliwataka wawekezaji wengine ndani ya Mkoa kuiga mfano wa KEDS,kwa kujitoa kusaidia vitakasa mkono, barakoa kwani mahitaji bado ni makubwa.
“Viwanda tunavyo vingi ,wawekezaji na wadau wengi tuendelee kujitoa kusaidia maeneo muhimu ambayo yanauhitaji wa tahadhali ya huu ugonjwa”
“;Ninawaomba pia wananchi waendelee kufuata maelekezo ya wataalamu wetu kujikinga na kujilinda na ugonjwa wa corona kwa kuepuka mikusanyiko ,kushikana mikono ” alisisitiza Ndikilo.
Akikabidhi msaada huo ,mkurugenzi wa Kampuni ya KEDS Group Limited Ben Song alisema wametoa mchango huo kuunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano dhidi ya COVID 19 na wanatarajia kutoa msaada wa Barakoa (Masks)na Vitakasa Mikono (Sanitizer).