………………………………………………………………..
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya amefanya ziara katika taasisi zilizo chini ya wizara yake ili kuona utekelezaji wa kazi unavyoendelea. Katibu Mkuu Kusaya ametembelea Tume ya Taifa ya umwagiliaji( NIC), Mfuko wa taifa wa pembejeo( AGITF) na wakala wa hifadhi ya chakula ya taifa ( NFRA).
Katika ziara yake amesisitiza watumishi wa Taasisi hizo kufanya kazi kwa bidii,kufuata taratib , kanuni na sheria za kazi katika utumishi wa umma.Pia amewataka watumishi hao kujiendeleza kielimu kwa kusoma kozi fupi na ndefu ili kuongeza ujuzi katika kazi zao kulingana na fani mbalimbali walizonazo.
“Watumishi tubadilike na tufanye kazi kwa bidii na yeyote atakayekwamisha miradi
yetu isiendelee nitamfukuza kazi” alisema Katibu Mkuu
Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhe. Kusaya amesema kwamba ni vyema kukawa na miradi michache ambayo Tume itaweza kuiendesha kuliko kuwa na miradi mingi ambayo haina tija. Mhe Kusaya aliyasema hayo baada ya kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bwana Nicodemus Kaal kwamba Tume ina miradi 2678 ambayo ipo sehemu mbalimbali kama Mombo, Moshi na Kilimanjaro.
“Tuwe na miradi michache ambayo tutaimaliza,kwenye utawala wangu lazima miradi yote iishe,kati ya hiyo miradi 2678 utakuta labda miradi 10 ndio imekamilika” alisisitiza Mhe.Kusaya
Aidha,amemtaka Mhasibu kuleta ripoti ya mitambo yote 56 ambayo ipo na malori 37 na sababu ya mitambo hiyo kutokukamilika kwa wakati na gharama ambazo wanawalipa wakandarasi hao.