Home Mchanganyiko NAISINYAI WATEKELEZA MAAGIZO YA SERIKALI YA KUJIKINGA NA CORONA

NAISINYAI WATEKELEZA MAAGIZO YA SERIKALI YA KUJIKINGA NA CORONA

0

Mwenyekiti wa Kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Merika Makeseni (katikati) akizungumzia na waandishi wa habari namna wananchi wa eneo hilo wanavyopambana na maambukizi ya virusi vya corona.

………………………………………………………………………………………..

WAKAZI wa Kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametekeleza maagizo yaliyotaolewa na serikali ya namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.

Mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai, Merika Makeseni akizungumza na waandishi wa habari jana alisema wananchi wa eneo hilo wamekuwa na mwamko mkubwa katika kujikinga na maambukizi hayo ya corona.

Makeseni alisema wananchi hao wametekeleza hayo kwa kuhakikisha wananawa kila mara kwa maji yanayotiririka na sabuni na kuepuka kusalimiana kwa mikono.

Alisema mwitikio wa kuepuka maambukizi ya virusi hivyo ni mkubwa kwa jamii hiyo kwani elimu ya namna ya kujikinga na corona wameipata na sasa wanaitekeleza.

“Wananchi wa Naisinyai wanatekeleza yale yote yaliyoelekezwa na serikali juu ya kujikinga na maambukizi hayo akiwemo Rais John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu,” alisema.

Alisema hata nyumba za ibada na sehemu za biashara ikiwemo maduka, saluni na migahawa midogo wameweka ndoo za maji na sabuni milangoni ili wanawe mikono.

Alisema hata kwenye sikukuu ya pasaka na jumatatu ya pasaka wakazi wa eneo hilo walioenda makanisani wamefuata utaratibu wa kutokukaribiana na kunawa mikono kabla ya kuingia na kutoka.

“Tunashukuru viongozi wa kimila, wazee wetu na wananchi kwa ujumla wanayaishi maneno yote yaliyoelekezwa kwao juu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona,” alisema Makeseni.

Alisema ni matarajio yake kuwa yake ni kuona wananchi wa eneo hilo wanaendelea kujikinga na maambukizi hayo kwa kufuata maelekezo ya serikali.