Home Mchanganyiko UMOJA WABAJAJI  (UMBI )WATOA MSAADA KWA WATOTO WANAOISHI MAZINGIRA MAGUMU

UMOJA WABAJAJI  (UMBI )WATOA MSAADA KWA WATOTO WANAOISHI MAZINGIRA MAGUMU

0

Mwenyekiti wa Umoja wa waendesha bajaji, Norbet Sumka akikabidhi moja ya misaada mbalimbali kwa Sister, Winfrida Mhongole wa kituo cha kulelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Tosamaganga

Mwenyekiti wa Umoja wa waendesha bajaji, Norbet Sumka akikabidhi moja ya misaada mbalimbali kwa Padre Franco Sordella ‘ Mwakilasi’ kwa ajili ya kituo cha watoto wanaoishi mazingira magumu cha Faraja Care Center (picha na Denis Mlowe)

…………………………………………………………………………………………….

NA DENIS MLOWE,IRINGA

KATIKA kuunga mkono mapambano dhidi ya ugonjwa Corona nchini Umoja wa Waendesha Bajaji Manispaa ya Iringa (UMBI) wamefanikiwa kutoa msaada kwa vituo viwili vya watoto wanaoishi katika mazingira magumu msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh milioni 3

Akizungumza  mara baada ya kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Umoja huo, Norber Sumka alisema kuwa lengo la msaada huo ni kuungana watoto katika kipindi hiki kigumu cha mapambano dhidi ya virusi vya Covid 19 kwani watu wengi wamejisahau kama kuna watoto hawa wanahitaji msaada wa vitu mbalimbali.

Alisema kuwa baada ya kuwatembelea na kubaini changamoto ambazo wanakabaliana walikaa kama uongozi na kuchangishana na wadau mbalimbali wakiwemo madereva wote wa bajaji na kuweza kupata vitu mbalimbali ambavyo wamekabidhi kwa vituo vya watoto wanaoishi katika mazingira magumu vya Tosamaganga na Faraja Care Center vilivyoko manispaa ya Iringa.

Alisema kuwa vitu ambavyo wamefanikiwa kutoa ni magodoro, unga wa ugali, mchele, nguo, sukari, sabuni, nepi kwa ajili ya watoto, matunda mbalimbali ambapo vitu hivyo vimegaiwa kwa vituo hivyo viwili vikiwa na thamani ya zaidi ya sh milioni 3.

Alisema kuwa kupitia utaratibu huo wa kurudisha faida katika jamii ametoa wito kwa wadau wengine kujitoa katika kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwani kwa kipindi hiki cha ugonjwa wa corona hali ya vituo hivyo ni ngumu na kuwafanya wazidi kuishi kwa shida.

Kwa upande wake, Katibu wa UMBI, Salum Gerald alisema kuwa Corona wanakabiliana na njia nyingi licha ya elimu kubwa inayotolewa na serikali kwa upande wao wamebaini kwamba watoto hao wanahitaji mahitaji mbalimbali kutokana na mazingira wanayoishi

Alisema kuwa kitendo cha serikali kufunga shule na watoto hao kurudi katika vituo ina maanisha kwamba wako tayari karantini hivyo jukumu letu kama jamii kuwasaidia chakula na vitu mbalimbali kuweza kupunguza changamoto wanazokabiliana nazo wakiwa ndani ya vituo wanavyolelewa.

Alisema kuwa jamii inapaswa kutambua na kujitoa katika kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kuwajali kwa kila namna ili waweze kuishi kwa upendo kama ambapo wangekuwa katika familia zao hivyo msaada huo utawasaidia kwa kiasi kidogo.

“Japo msaada sio mkubwa sana kukidhi mahitaji ya watoto yatima,bali itasaidia  kidogo kufanya watoto wajisike wapo kama watoto wengine wenye wazazi kwani kutoa ni moyo hivyo ni wakati huu wa mapambano dhidi ya corona kuna umuhimu mkubwa sana kwa watu kujitolea vitu mbalimbali kwa watoto hawa” alisema

Alisema kuwa watoto yatima ni wahanga wa matatizo yetu katika jamii ndio maana wapo hivyo sio jukumu la serikali pekee kuwahudumia watoto hawa kutokana na umuhimu wao katika jamii kwani ndani yao kuna watoto watakaokuja kuwa kuwa Profesa, madaktari bingwa na wanasheria hivyo kuwatembelea ni njia mojawapo ya kuwafanya wapate moyo wa kusoma zaidi na kujitoa.

Kwa upande wao viongozi wa vituo hivyo, Father, Franco  Sordella wa kituo cha Faraja na Sister  Winfrida Mhongela wa kituo cha Tosamaganga walishukuru umoja wa bajaji kwa kuwakumbuka kwa misaada hiyo na imekuja kwa wakati mwafaka kutokana na changamoto nyingi ambazo wanakabiliana nazo katika vituo.

Walisema kuwa kitendo cha UMBI kuwakumbuka kwa misaada hiyo wakati dunia nzima inapambana na Corona na misaada ya wadau mbalimbali inakwenda huko hakika ni faraja tosha kabisa kwa watoto ambao wamekuwa wakisaulika na jamii kwa kudhani vituoni wanapata kila kitu.

Father Franco alisema kuwa licha ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ndani ya kituo kuhusu watoto alisema kuwa changamoto kubwa kituoni hapo ni suala la umeme na maji ambapo umeme alipofatilia kwa kipindi cha miaka mitatu ni gharama kubwa kuliko matarajio yao ambapo milioni zaidi ya 52 alizotajiwa na shirika zilimshinda.

Kwa upande wake Sister Winfrida Mhongole alisema kuwa changamoto kubwa katika kituo hicho ni baadhi ya walezi hawaji kuwasalimia wala kuwachukua watoto sasa tunapata shida wakati wanapotakiwa kurudi nyumbani, maana umri wa mwisho wa kukaa kituoni hapa ni miaka 6.

Alisema kituo kinapokea watoto wasio na mama au wenye mama ambaye ni anatatizo la akili, na kuwa baadhi ya ndugu ndiyo wamekuwa wakiwatelekeza watoto mara tu wanapowafikisha kituoni hapo.

Changamoto nyingine zinazowakabili watoto ni baadhi ya wazazi kushindwa kuwaendeleza kielimu watoto, kwani baadhi ya walezi huwa hawana mwamko wa kuwaendeleza watoto hao, na hivyo kusababisha watoto hao kutoendelea na masomo

Vituo hivyo ambavyo jumla  vina watoto zaidi ya 240 kwa kuwa kituo cha Tosamaganga pekee kina watoto 180 ambapo wanaishi kwenye vituo hivyo huku kituo cha faraja kina watoto zaidi 60 ambao wanaishi katika vituo hivyo na kuhitaji msaada wa vitu mbalimbali.