Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb) akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa MKURABITA kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za
Mitaa wakati wa ziara ya kamati hiyo mkoani Singida yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali mkoani Singida.
Baadhi ya Wafanyabiashara wanaofaidika na uwepo wa Kituo cha Pamoja cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara, Manispaa ya Singida, wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Dkt. Jasson Rweikiza (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao leo wakati wa ziara ya kamati yake mkoani humo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali mkoani Singida.
Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Biashara na Rasilimali za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Dkt. Seraphia Mgembe akitoa ufafanuzi kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wa namna MKURABITA
ilivyoshiki katika uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara, Manispaa ya Singida wakati wa ziara ya kamati hiyo mkoani Singida yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali mkoani
humo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Dkt. Jasson Rweikiza (Mb), akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Biashara wa Manispaa ya Singida, Bw. Erick Simkwembe ya namna Kituo cha Pamoja cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara, Manispaa ya Singida kinavyofanya kazi.
Mfanyabiashara wa Manispaa ya Singida, Bi. Happy Francis akitoa maelezo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusiana na bidhaa anazozalisha wakati wa ziara ya kamati hiyo mkoani Singida yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali mkoani humo.
****************************
James Mwanamyoto – Singida
Tarehe 13 Machi, 2020
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imeipongeza MKURABITA na Manispaa ya Singida kwa kuanzisha Kituo cha Pamoja cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara ambacho kimewezesha mchakato mzima wa urasimishaji wa biashara kuwa wa haraka, rahisi na wa gharama nafuu kwa wafanyabiashara wanyonge.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Jasson Rweikiza (Mb) mara baada ya Kamati yake kufanya ziara katika kituo hicho na kushuhudia namna kinavyowasaidia wafanyabiashara wanyonge kurasimisha biashara zao.
“Nimefurahishwa na utendaji kazi wa kituo hiki ambacho kinawasaidia wananchi kuondokana na umaskini kupitia urasimishaji wa biashara zao jambo ambalo ndio lengo
kuu la Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge,” Mhe. Dkt. Rweikiza amefafanua.
Mhe. Dkt. Rweikiza ametoa wito kwa wananchi wa Manispaa ya Singida kukitumia ipasavyo kituo hicho ili kuboresha maisha yao.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb), amepongeza ushirikiano mzuri uliopo kati ya MKURABITA na Manispaa ya Singida uliowezesha uanzishwaji wa kituo hicho kilichowapunguzia usumbufu wafanyabiashara ambao kwa sasa wanapata huduma za urasimishaji na uendelezaji biashara sehemu moja.
Mhe. Mkuchika ametoa rai kwa halmashauri zote nchini kuanzisha vituo vya huduma ya pamoja vya urasimishaji biashara ili kuwasaidia wananchi kujikwamua na umaskini.
Akizungumzia umuhimu wa uanzishwaji wa kituo hicho, Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe amewataka wananchi kupata huduma katika kituo hicho na
kumtumia Afisa Biashara kikamilifu ili kuwaongoza katika mchakato wa kurasimisha biashara zao.
Aidha, Dkt. Mgembe amewataka wananchi kuwasilisha changamoto za kibiashara wanazokabiliana kwa Afisa Biashara wa Kituo hicho ili zitafutiwe ufumbuzi, na kuongeza kuwa, MKURABITA iko tayari kuzifanyia kazi changamoto zote zinazojitokeza kwa ajili ya kufanya maboresho.
Kituo cha Pamoja cha Urasimishaji na Uendelezaji Biashara katika Manispaa ya Singida kilianza kutumika tarehe 10/12/2019 ambapo huduma mbalimbali za urasimishaji na uendelezaji biashara katika Manispaa hiyo zinatolewa na Maafisa kutoka Manispaa ya Singida, TRA, SIDO na Benki ya NMB.