Bw. Bernrad Dadi Mkurugenzi wa Mfumo wa Malipo wa Taifa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) aktoa mada kuhusu Kanzidata ya Kudumu ya Watoa Huduma za Kifedha Financial Services Register (FSR) katika semina ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari inayoendelea kwenye tawi la BoT jijini Arusha leo.
Bw. Augustine Hotay Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki Benki Kuu ya Tanzania (BoT) akitoa mada kuhusu matumizi safi ya Noti na utambuzi wa alama muhimu zilizopo katika Noti.
Zalia Mbeo Meneja Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki (BOT) akizungumza na washiriki wa semina ya Uchumi na Fedha inayoendelea kwenye tawi la BoT jijini Arusha.
Baadhi ya waandishi wa habari wanaoshiriki katika semina hiyo wakiangalia alama muhimu zilizopo kwenye Noti ya Shilingi elfu 10.000.
………………………………………..
Benki Kuu ya Tanzania BoT imeanzisha mfumo mpya wa huduma za kifedha kwa kushirikiana na wadau wengine ambao ni CDC, TIRA TCDC CMSA na TAMISEMI ili kutengeneza Kanzitada itakayowaorodhesha watoa huduma wote wa shughuli za Kifedha.
Bw. Bernrad Dadi Mkurugenzi wa Mfumo wa Malipo wa Taifa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) amesema hayo mara baada ya kutoa mada kuhusu Kanzidata ya Kudumu ya Watoa Huduma za Kifedha Financial Services Register (FSR) katika semina ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari inayoendelea kwenye tawi la BoT jijini Arusha leo.
Amesema hapo mwanzo BoT ilikuwa ikipata taarifa au data kwa kutumia tafiti ambazo zilikuja kuonekana zina mapungufu kwasababu zilikuwa zinachukua muda kupatikana lakini pia ilikuwa ni gharama kubwa kwa sababu ili kupata hizi data au taarifa ilibidi kuajili kampuni au kikundi ili kutapita nchi nzima ili kukusanya taarifa hizo.
Amesema Mwaka 2012 na 2014, tafiti mbili za kijiografia za maeneo ambayo huduma za kifedha
hupatikana zilifanyika Tanzania na FSDT kwa niaba ya Benki kuu ya Tanzania, ukiangalia hapo utagundua ni kipindi cha mwaka mzima ulipita hivyo utaona hapa katikati kulikuwa na watoa huduma ambao hawakusajiliwa.
Ameongeza kuwa jambo lingine lilikuwa ni kwamba taarifa hizi ziko maeneo mbalimbali, Kwa mfano ili kujua mawakala wa bima ilibidi lazima uende TIRA kupata taarifa zao, Ili kujua mawakala kampuni za simu ilibidi kwenda Tigo, Vodacom, Airtel na kadhalika na ukitaka kupata taarifa za SACCOS ilibidi pia uende kwenye SACCOS zao , hivyo ilikuwa vigumu sana kupata taarifa sahihi.
Bw. Bernrad Dadi amesema hili ndilo lililofanya wasimamizi wa huduma za fedha BoT na wadau wengine kama CDC, TIRA TCDC CMSA na TAMISEMI kukaa pamoja na kutengeneza Kanzitada hiyo ambayo iitatupa faida Watunga sera kujua wapi huduma hazijafika, Wawekezaji kujua wapi hawapo hapa nchini ili kujipanga kupeleka huduma sehemu ambazo hawapo. Lakini pia kuwajua watoa huduma za kifedha wakubwa na wadogo popote walipo na shughuli wanazofanya.
“Wasimamiiaji wa huduma hizi hatuna tena sababu ya kwenda Tigo , Halotel, Vodacom na maeneo mengine ili kujua ana mawakala wangapi, taarifa hizo tutakuwa tunazipata kwa pamoja na kuzitoa kwa pamoja . pia itasaidia katika utekelezaji wa Sera za nchi ambazo tunaita (National Financial Inclussion Framework) ambazo zinatekelezwa”. Amesema Bw. Dadi.
Ameongeza kuwa utengenezaji au uundaji wa Kanzidata yenyewe umeshakamilika kwa asilimia 98 yamebaki mambo ya taarifa mbayo watumiaji watatuambia na kushauri namna ya kuziweka taarifa hizo.
Usajili wa watoa huduma hao awamu ya kwanza utaanza mwezi huu wa Machi na Aprili ambapo na awamu ya pili ya usajili huo itafanyika mwezi Mei na Juni mwaka huu.
Ameongeza kuwa itakapofika Julai Mosi mwaka huu mfumo huu utakuwa uko tayari na una taarifa zote , baada ya hapo wataachiwa watoa huduma wakubwa ambao wataendelea kuwasajili watoa huduma wapya kadiri watakavyoandikisha, baada ya hapo tutakuwa tunawajua watoa huduma wote wakubwa na wadogo nchini.
Amesema ukishawaunganisha watoa huduma hao na mifumo mingine kama vile Tanzania InteBank Payment System (TIPS) utakuwa na uwezo wa kujua hela hizi zimetoka mkoa huu na kwenda mkoa huu na kwa kutumia Kanzidata hii tutajua na kupata takwimu sahihi za miamala ya fedha iliyofanyika na kuleta ufanisi wa huduma za kifedha nchini .