Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi,akizungumza kabla ya mgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kuzindua shule shikizi ya Msingi Chiwondo iliyopo kata ya Nala jijini Dodoma.
…………………………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
KATIKA kuongeza motisha ya ufundishaji, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi ameahidi kuwapatia pikipiki walimu ambao wamekua wakitembea umbali mrefu kwenda mashuleni.
Kunambi ametoa ahadi hiyo leo katika uzinduzi wa shule ya msingi Mavunde ambayo imejengwa kwa ushirikiano wa Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde na Halmashauri ya Jiji hilo.
Akizungumza mbele ya mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Kunambi amesema kwa kutambua changamoto ambayo walimu hao wamekua wakipitia ofisi yake itatoa pikipiki mbili kwa walimu hao ili ziweze kuwasaidia kufika shuleni na kurudi majumbani mwao.
” Mhe Waziri walimu wetu hawa wawili ni wazalendo haswa. Kila siku wamekua wakitembea kilomita 20 kwa miguu kuja hapa kufundisha watoto wetu na kurudi majumbani mwao na hata siku moja hawajawahi kunung’unika.
Kama Mkurugenzi wa Jiji nimeguswa na moyo wa kizalendo walionao walimu hawa na nimeona niwapatie pikipiki ambazo kwa hakika zitawasaidia kufika shuleni kwa wakati bila kuwa na uchovu jambo ambalo naamini licha kuwa kama motisha pia litaongeza ufanisi wao katika ufundishaji,” Amesema Mavunde.
Mkurugenzi huyo pia ameahidi kujenga jengo la utawala kwenye shule hiyo sambamba na nyumba za walimu hao ili kuondoa kabisa changamoto ya kutoka umbali mrefu kufika shuleni.
Amesema ndani ya kipindi cha miaka minne Jiji hilo limejenga madarasa 188 kwa pato la ndani huku pia ufaulu ukiongezeka kutokua kuwa Halmashauri ya 67 hadi kuwa ya 38 katika matokeo ya kidato cha nne.
” Mhe Waziri Jiji hilo Hatuwezi kusema linafanya vizuri sana kwenye elimu lakini ni wazi tumekua tukipiga hatua kubwa kulinganisha na miaka ya nyuma. Lengo letu ni kuhakikisha elimu inakua kwa kasi kwenye Jiji letu kama ambavyo tumekua tukikua kwenye sekta zingine.
Tunafahamu Rais wetu amekua akilipa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya sera ya elimu bila malipo, na sisi tunaahidi kuendelea kuboresha miundombinu na kuweka mazingira rafiki kwa walimu na wanafunzi wetu ili tuweze kufanya vizuri zaidi na kuakisi maana ya kuwa Makao Makuu ya Nchi na Serikali,” Amesema Kunambi.