NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
VIJIJI 10,446 nchini vinatarajia kufikiwa na umeme huku asilimia zaidi ya 70 ya vijiji vilivyopo mkoa wa Pwani ,vikiwa vinatarajia kufikiwa na huduma hiyo ifikapo June mwaka huu.
Aidha vijiji 1,822 vitabakia ambavyo vitafikiwa na umeme kupitia
mradi wa REA awamu ya III mzunguko wa pili ambao kazi itaanza mwezi Februari mwaka huu.
Hayo aliyabainisha, Naibu Waziri Wa Nishati, Subira Mgalu ,wakati akielezea kuhusu mradi wa REA awamu ya III mzunguko wa kwanza unaotarajia kukamilika June 2020 ,katika ziara yake ya kutembelea kujionea kazi inayofanywa na mkandarasi Sengerema eneo la Kibindu na Talawanda jimbo la Chalinze ,mkoani Pwani.
Alisema, katika kutekeleza mradi huo baadhi ya maeneo hayakukamilika mapema kutokana na wigo kuwa mdogo,hivyo serikali ya awamu ya tano ilikubali kuidhinisha takriban kilometa 3,000 za ziada ili kukidhi orodha iliyotajwa kwenye REA awamu ya III mzunguko wa kwanza,mradi utakaogharimu sh.bil 164 .
Subira alifafanua, kutokana na hatua hiyo vijiji 3,559 viliorodheshwa katika mzunguko huo ikiwemo vijiji vinne vya kata ya Kibindu na vitatu kata ya Talawanda mkoani Pwani.
Alielezea, eneo la Talawanda ni muhimu kwani lipo karibu na Chalinze ,ambapo kunajengwa mradi mkubwa wa kituo cha kupokea na kupoza umeme unaotoka Rufiji -Stigo -Chalinze ,njia ya Kinyerezi -Chalinze na Chalinze -Dodoma.
“Nimeridhishwa na kazi inayoendelea, mkandarasi anastahili pongezi, na nawashukuru wizara ya fedha kwa kuidhinisha fedha ongezeko la fedha hiyo”
“Nitoe rai kwa wananchi kujipanga kuweka nyaya za umeme na kuunganishiwa umeme kwa gharama ndogo ya sh.27,000 sawa na debe tatu ama mauzo ya kuku wawili au watatu”alifafanua Subira.
Subira alisema, mahitaji ni makubwa na sekta ya nishati imepiga hatua kwani hadi sasa asilimia 69 ya vijiji 12,268 vimefikiwa na umeme, na kazi inaendelea .
Subira alisema ,utekelezaji wa ilani 2015-2020 watakamilisha malengo yao na kitakachobakia ni 2020-2025 kufikia vitongoji na kazi kubwa itakuwa ni usambazaji.
Mbunge wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete alieleza ,awali kata ya Kibindu haikuwa sehemu ya mradi wa REA .
Ridhiwani alisema, baada ya kuomba na mazungumzo ,kupitia serikali ya awamu ya tano iliyo sikivu kata hiyo ikawa miongoni mwa kata zilizotengewa fedha kwa ajili ya mzunguko huu.
Awali diwani wa kata ya Kibindu ,Ramadhani Mkufya alisema,kupata umeme Kibindu ni maendeleo na uchumi unakwenda kukua tofauti na miaka mingi ya nyuma ambayo umeme haukuwepo.
Nae diwani wa Talawanda ,Saidi Zikatimu alimwambia ,Subira kwamba kijiji cha Ludiga kina mahitaji makubwa ya umeme kwakuwa kina wakazi wengi 4,416 na kaya 526 ,pamoja na kijiji cha Kisanga na Mindukene.