Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Lupungwi wilayani Bagamoyo mara baada kufika kijijini hapo kwa ajili ya ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme kijijini humo.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akisaini kitabu cha wageni mara baara ya kufika kwenye mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Kimange wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Tanesco Mkoa wa Pwani Martin Madulu mara baada ya kufika wilayani humo kukagua kazi ya usambazaji umeme.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(wa kwanza kushoto) akiwa kwenye kituo cha afya cha Kimange wilayani Bagamoyo pamoja na viongozi mbalimbali wa kijiji hicho wakati alipokwenda kukagua kazi ya usambazaji umeme kwenye taasisi za umma.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kimange wilayani Bagamoyo mara ya baada ya kukagua kazi ya usambazaji umeme kijijini humo.
Wananchi wa kijiji cha Talawanda wilayani Bagamoyo wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu( hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo wakati Naibu Waziri alipofika kijijini hapo kukagua kazi ya usambazaji umeme.
……………….
Hafsa Omar – Pwani
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amesema kazi ya kusambaza umeme nchini ni endelevu na Serikali inatarajia kuanza rasmi kusambaza umeme kwenye vitongoji vyote nchini mara tu baada ya kumaliza kusambaza umeme kwenye vijiji vyote ifikapo Juni 2021.
Aliyasema hayo, Januari 21, 2020, kwa nyakati tofauti akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme katika vijiji vya Kimange, Kibindu, Lupungwi na Talawanda, wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Alisema jukumu la Serikali ni kutoa huduma kwa wananchi wake na Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kutoa huduma ya nishati ya umeme kwa Watanzania wote.
“ Kazi ya kupeleka umeme vijijini tunaikamilisha mapema Juni 2021, kazi inayofuata ni kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote nchini kwahiyo ni kazi ya kata mti panda mti.” Alisema
Pia, aliwataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuunganisha umeme kwenye nyumba zao, kwasababu Serikali inatumia fedha nyingi kuhakikisha miundombinu ya umeme inafika sehemu zote bila kuangalia umbali wa maeneo.
Aliongeza kuwa, maeneo mengi ya Chalinze, mara ya baada kusambaziwa umeme wawekezaji wengi wamejitokeza kuwekeza kwenye maeneo hayo ambapo hapo awali walishindwa kufika katika maeneo hayo kwasababu ya changamoto ya upatikanaji wa umeme lakini kwasasa fursa nyingi za kiuchumi zimejitokeza wilayani humo.
Mgalu, aliendelea kuwahimiza viongozi mbalimbali wa Halmashauri, Wenyeviti na Madiwani kuendelea kutenga fedha za kuunganisha umeme kwenye Taasisi za umma na kwamba suala hilo ndio liwe kipaumbele chao mara tu baada ya miuondombinu ya umeme kufika kwenye maeneo yao.
Aidha, alilipongeza Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) kwa kazi nzuri wanayoifanya ya usambazaji umeme, na kumtaka Meneja wa Mkoa huo kuhakikisha hakuna kijiji kitakachorukwa kwenye mradi wa REA III, ili wananchi wote wafaidike na huduma hiyo.