Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Dkt John Jingu,akizungumza wakati wa mkutano wa kutathmini kuhusu maboresho ya sera ya wazee ya mwaka 2003 jijini Dodoma.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi akielezea jambo wakati wa mkutano wa kutathmini kuhusu maboresho ya sera ya wazee ya mwaka 2003 kilichofanyika leo jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Dkt John Jingu,akionyesha kitabu cha taarifa ya mapitio ya sera ya taifa ya wazee ya mwaka 2003 wakati wa mkutano wa kutathmini kuhusu maboresho ya sera ya wazee ya mwaka 2003 kilichofanyika leo jijini Dodoma.
……………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Dkt John Jingu amesema wameamua kupunguza makazi ya wazee kutoka 17 hadi kufikia 13 ili kuboresha huduma na kutoa huduma Bora zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma mara baada ya mkutano wa kutathmini kuhusu maboresho ya sera ya wazee ya mwaka 2003 uliohusisha Taasisi na Idara za Serikali ili kuona kama inapaswa kuboreshwa au laa.
Dkt Jingu amesema wameamua kupunguza makazi hayo Kutokana na kutaka kuboresha na kuimarisha ufanisi katika kuwahudumia Wazee ili wapate huduma zilizo bora.
” Makazi yaliyopunguzwa ni pamoja na Chanzi (Morogoro),Ngehe (Ruvuma),Nandanga (Lindi) ,Mkaseke (Mtwara), tumefanya hivyo ili kuboresha huduma kwa wazee” amesema Dkt Jingu.
Ameongeza kuwa “tunalo jukumu Kama Serikali kuwahudumia kila kitu lakini halizuii familia zenye uwezo wa kuwahudumia wazee katika familia ambazo Wazee hao wanatoka, “amesema.
Amesema hivyo familia zinapaswa kuwaangalia wazee kwa jukumu hilo ni la kwao mbali na hilo wamesisitiza kuwepo kwa mabaraza ya wazee ili kusaidia changamoto mbalimbali ambazo zinatokea katika maeneo mbali mbali hapa nchini.
Katika hatua nyingine amebainisha wazee takribani 680 wamepatiwa msaada na Serikali kupitia mfuko wa kunusuru Kaya maskini TASAF ili kuongeza mitaji yao katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kwa upande wake Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi ,amesema kuangalia muda tayari inatosha kufanyiwa marekebisho.
Amesema tayari wameshaandaa rasimu ambayo wanakwenda kuitengeneza yakiwemo matamko ambayo yanakwenda kufanyiwa Kazi ndani ya siku ambazo watakuwa katika kikao hicho.
Naye mmoja wa Wazee waliohudhuria kikao hicho Mzee Abdalah Majumba kutoka Lindi amesema wazee wanapaswa kuheshimiwa hivyo kunapaswa kuwepo na sheria ambayo itawaelekeza jamii kufanya hivyo ili kumsaidia Mzee.
“Unakuta kwenye daladala au sehemu nyingine wazee wanasimama hadi wanadondoka hakuna anayempisha lakini ikiwepo sheria yote yatawezekana, “amesema Majumba.
Naye Clement Sherenguzi amesema kuna haja ya kufanyiwa marekebisho ya sera hiyo ili nao wapate mwanga, hata hivyo ameshukuru kwa serikali kushughurikia maswala ya mauaji kwa Wazee ambayo yalikuwa yakiwapa hofu.