Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Zanzibar, Mhe. Harusi Saidi Suleiman, Mwakilishi wa Jimbo la Wete akisaini Kitabu cha wageni alipotembelea Banda la TAEC katika viwanja vya Maisara Zanzibar
Bw. Ali Masoud mtumishi wa TAEC akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la TAEC katika viwanja vya Maisara, Zanzibar
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) inashiriki kikamilifu maonesho ya elimu na biashara yaliyofanyika viwanja vya maisara mjini Zanzibar. Hii ni mara ya pili kwa TAEC kushiriki maonesho haya kisiwani Unguja, maonesho haya uandaliwa maalumu kila mwaka katika kuadhimisha sikukuu ya Mapinduzi ambapo kwa mwaka huu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inaadhimisha miaka 56 tangu ilipotokea mapinduzi hayo mwaka 1964.
Maonesho haya ya siku kumi na nne (14) yalianza rasmi tarehe 02 Januari, 2020, ambapo yalizinduliwa rasmi tarehe 07 Januari, 2020 na Mhe. Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo kilele chake ni tarehe 15 Januari, 2020 ndipo yatakafungwa rasmi. Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ndio iliyoratibu maonesho haya ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
TAEC imekuwa ikishiriki katika maonesho haya maalum ili kutoa elimu juu ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na TAEC kisheria ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku lengo kuu likiwa ni kusikiliza na kujibu changamoto za wafanyabiashara na utaratibu mzima wa utolewaji wa vibali vya uingizaji na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi.
Katika zoezi hili TAEC imeainisha sababu mbalimbali muhimu za upimaji wa bidhaa katika mnyororo wa chakula ambapo wananchi na wafanyabishara wameelezwa kwa kina juu ya sababu za upimaji wa bidhaa hizo, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa mionzi katika mnyororo wa bidhaa ili kulinda watanzania dhidi ya madhara hatari yanayoweza kusababishwa na mionzi kutokana na kwamba nchi imeshakumbwa na matukio ya usafirishwaji usio rasmi wa vyanzo vya mionzi (illicit trafficking of radiaoactive sources) ambapo kama ikitokea vyanzo hivyo vikaingia katika mnyororo wa bidhaa Taifa zima litakuwa katika hatari.
Wananchi na wafanyabiashara pia wameelezwa juu ya uwepo wa mionzi katika mazingira kutokana na uwepo wa madini ya urani nchini mwetu kwamba ni sababu nyingine ya msingi ya TAEC kulazimika kupima mionzi katika mnyororo wa bidhaa ili kuhakikisha bidhaa zote ziko salama dhidi ya chembechembe au viasili vya mionzi.
Pia wananchi wamejulishwa kuwa wajibu mkubwa wa serikali ni kulinda wananchi, hivyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina wajibu wa kulinda wananchi wake dhidi ya madhara yatokanayo na mionzi, ndiyo sababu imechukua hatua za kulinda mnyororo mzima wa chakula ili wananchi wake wabaki kuwa salama.
Wakati wa uzinduzi wa kriniki ya biashara iliyozinduliwa tarehe 10 Januari, 2020 na Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa Viwanda na Biashara, Wananchi wamejulishwa kuwa kutokana na changamoto mbalimbali za kibiashara zinazojitokeza duniani, serikali iliamua kuchukua jukumu la kulinda soko la bidhaa zetu zinazouzwa nje ya Tanzania hasa wakati huu wa vita ya kiuchumi kwa kuzipima na kujiridhisha kuwa ni salama kabla ya kuzisafirisha ili isije kutokea kwa namna yoyote ile watu wasio waaminifu wakazichafua kwa makusudi ili bidhaa zetu zisipate soko, hivyo upimaji wa mionzi katika bidhaa zetu unatoa uwezekano wa kufuatilia kama kuna shida yoyote na kuchukua hatua zaidi.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Zanzibar, Mhe. Harusi Said Suleiman, alipotembelea banda la TAEC alijulishwa juu ya takwa la kisheria la kupima mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa kama ilivyoahinishwa kwenye Sheria Na. 7 ya Mwaka 2003, kuwa Sheria hii inaendana na matakwa ya kimataifa ikiwemo shirika la afya duniani (WHO), shirika la kilimo na chakula duniani (FAO), na shirika na nguvu za atomu duniani (IAEA) katika kuhakikisha mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa inadhibitiwa ili kuzuia madhara ya mionzi yanayoweza kujitokeza.
Wakati huo huo Mhe. Bi. Harusi ameitaka TAEC kufika katika Hospitali ya Mnazi mmoja ambayo kwasasa wako katika hatua za mwisho za kufunga mashine za CT-Scan ili kufanya ukaguzi kabla ya hatua hizo kukamilika. Mhe alijibiwa ya kuwa hatua za awali za ukaguzi zilifanyika na zoezi lingine litaendelea mara mashine hizo zitakaposimikwa.