Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kufungua mkutano uliowakutanisha wakandarasi wazawa
na wadau wa ujenzi, jijini Dodoma, kushoto ni Mkurugenzi mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.
Wakandarasi wazawa na wadau wa ujenzi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, katika mkutano uliowakutanisha Katibu Mkuu huyo,
wakandarasi wazawa na wadau wa ujenzi, jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Miradi ambaye amemwakilisha Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Crispianus Ako, akifafanua jambo katika mkutano uliowakutanisha wakandarasi wazawa na wadau wa
ujenzi, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akisisitiza jambo katika mkutano uliowakutanisha Katibu Mkuu huyo, wakandarasi wazawa na wadau wa
ujenzi, jijini Dodoma.
PICHA NA WUUM
************************************
Serikali imesema itashirikiana na Benki ya CRDB na benki nyingine zitakazokuwa tayari kuhakikisha inawasaidia wakandarasi wazalendo kupata fursa za mikopo ya haraka na nafuu ili kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi mikubwa inayotekelezwa nchini.
Hayo yamesema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, katika mkutano wa wakandarasi wazawa na wadau mbalimbali wa ujenzi, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Mwakalinga amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya wakandarasi wazawa ikiwa ni pamoja na kupitia na kuangalia upya baadhi ya maeneo yaliyo na utata ambayo yamo kwenye mikataba ya
miradi mbalimbali ili kuyaboresha na kwa kuanzia amesema Wizara yake itaangalia mikataba inayotekelezwa katika miradi ya ujenzi.
“Mkutano huu tumeuandaa lengo likiwa ni kuboresha maslahi ya wakandarasi wazawa kwani hii si mara ya kwanza kuanzisha kitu kama hiki, kutokana na umuhimu huo tumeamua kuishirikisha Benki ya CRDB na benki nyingine zitakazokuwa tayari ili kuwasaidia na hivyo kuwajenga na kuwaongezea uwezo wa kujenga miradi mikubwa hususani ya ndani ya nchi”, amesema Katibu Mkuu Mwakalinga.
Katibu Mkuu Mwakalinga, amefafanua kuwa tayari timu ya wataalamu kutoka Wizarani imeshapitia mikataba kadhaa na kuja na mapendekezo ya namna ya kuwasaidia wakandarasi wazawa kushiriki katika ujenzi wa
miradi mikubwa ikiwa ni utekelezaji kwa awamu ya kwanza.
Ameongeza kuwa awamu ya pili ya utekelezaji huo utahusisha wataalamu kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na wakandarasi wazawa ili kuja na mapendekezo
muhimu yatakayokidhi mahitaji ya sasa ya na siku zijazo katika sekta ya ujenzi.
Amewataka wakandarasi hao kutumia kikao hicho kujadili na kutoa maoni ambayo yatafanikisha mpango huo wa Wizara wa kuwasaidia wakandarasi hao.
Amesisitiza kupitia mpango huo hata Serikali kupitia CRB inaweza kupata Takwimu sahihi za wakandarasi ambazo zitajumuisha uwezo wa kiutendaji wa wakandarasi hao katika masuala ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema kupitia benki ya CRDB wakandarasi wazawa wataweza kunufaika kukuza mitaji yao na kumudu kutekeleza miradi mingi kwa wakati.
“Kuna maeneo ambayo tumeyaboresha ili kuhakikisha watanzania wananufaika na mikopo hiyo ikiwemo kwa wakandarasi hao kuwezeshwa kifedha ili kusonga mbele”, amesema Mkurugenzi Mkuu.
Mkutano huu ni Mkutano wa Tatu Kufanywa na Katibu Mkuu Mwakalinga, baada ya Mkutano wa tarehe 11 mwezi Juni na wa tarehe 20 mwezi Julai mwaka jana, lengo likiwa ni kujadili changamoto zinazowakabili wakandarasi wazawa nchini na kuzifanyia kazi.