Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Hospitali ya Rufaa ya Kusini wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Mtwara kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evord Mmanda na kulia ni Mkadiriaji Majenzi wa NHC Anania Sauden.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Hospitali ya Rufaa ya Kusini wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Mtwara kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evord Mmanda.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioneshwa ramani ya ujenzi wa wa jengo la Hospitali ya Rufaa ya Kusini na Mkadiriaji Majenzi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa Anania Sauden wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo jana akiwa katika ziara yake ya siku mbili mkoani Mtwara. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evord Mmanda.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitoa maelekezo kwa Msajili wa Hati Kanda ya Kusini Mpoki Mwalufunda katika halmashauri ya Nanyamba jana wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Mtwara kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evord Mmanda.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya Nanyamba mkoani Mtwara jana wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Mtwara kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwabana Maafisa Ardhi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Mtwara kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evord Mmanda.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia hati za ardhi zinazosubiri kukamilishwa kwa kusainiwa na wamiliki wake katika ofisi ya ardhi Manispaa ya Mtwara Mikindani jana wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Mtwara kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evord Mmanda.
………………………………………………
Na Munir Shemweta, WANMM MTWARA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameonesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara na kuagiza kuondolewa katika nafasi ya mkuu wa idara ya ardhi wa halmashauri hiyo Mariam Kimoro.
Uamuzi wa kumvua wadhifa wa ukuu wa idara ya ardhi katika Manispaa ya Mikindani unafuatia Mkuu huyo wa idara kushindwa kusimamia vyema ukamilishaji wa hati za ardhi 150 zilizoombwa na wamiliki wake kwa miaka tofauti kuanzia mwaka 2011.
Akizungumza katika manispaa hiyo jana wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Mtwara Dkt Mabula alisema haiwezekani hati za ardhi kuandaliwa tangu mwaka 2011 ambapo hadi sasa wamiliki wake wameshindwa kusaini kwa ajili ya kumilikishwa jambo alilolieleza linaikosesha pia serikali mapato.
‘’ Hatuwezi kuwa na Mkuu wa Idara asiyefanya kazi yake ipasavyo, anasubiri watu waje wasaini na hakuna jitihada zozote zilizofanyika kuwatafuta mmiliki wake na hata kuwapigia simu?’’ alisema Mabula.
Afisa Ardhi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Edna Chacha aliitetea idara hiyo kwa kueleza kuwa imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kukamilisha hati za ardhi lakini changamoto kubwa ni wamiliki wake kushindwa kujitokeza kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kumilikishwa.
Hata hivyo, Naibu Waziri Mabula alipingana na Afisa Ardhi huyo kwa kumueleza kuwa haiwezekani idadi ya wamiliki 150 kwa pamoja washindwe kupatikana kwa ajili ya kusaini ili wamilikishwe na kubainisha kuwa hali hiyo inachangiwa na uzembe wa idara hiyo kushindwa kuwafuatilia wamiliki hao
Dkt Mabula ambaye aliitembelea pia halmashauri za Mtwara na Nanyamba amezitaka idara za ardhi kwenye halmashauri za mkoa wa Mtwara kujipanga katika kushughulikia masuala ya ardhi ikiwemo kuingiza majalada ya ardhi kwenye mfumo wa kielektroniki kwa asilimia mia moja.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini iliyopo eneo la Mitengo katika mkoa wa Mtwara.
Ujenzo huo unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu na kugharimu takribana bilioni 15.8 unafanywa na shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na utahudumia mikoa ya kusini ya Mtwara, Songea, Lindi pamoja na nchi jirani ya Msumbiji.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa jengo hilo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amelipongeza shirika la Nyumba la Taifa kwa kujenga jengo hilo kwa kasi aliyoieleza kuwa italifanya jengo kukamilika kabla ya muda uliopangwa.
Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Mtwara Angelina Magazi alisema Shirika lake limejipanga kuhakikisha ujenzi wa jengo hilo unakamilika mapema na kubainisha kuwa ujenzi huo kwa sasa unafanyika usiku na mchana.
‘’ Lengo la kufanya kazi usiku na mchana ni kuhakikisha tunakamilisha ujenzi wa jengo hili la hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini mapema kabla ya muda tuliopewa kwani hayo ndiyo malengo yetu ya ndani kama Shirika’’ alisema Magazi.